Ukarabati Kisima cha Songosongo kuongeza uzalishaji gesi asilia

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 08:40 PM Oct 28 2024
Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Charles Sangweni (mwenye fulana nyeusi) akiwa kwenye ziara maalumu katika Kitalu cha Songo Songo Mkoani Lindi ambapo kazi ya ukarabati wa kisima cha uzalishaji wa gesi asilia inaendelea.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Charles Sangweni (mwenye fulana nyeusi) akiwa kwenye ziara maalumu katika Kitalu cha Songo Songo Mkoani Lindi ambapo kazi ya ukarabati wa kisima cha uzalishaji wa gesi asilia inaendelea.

UKARABATI wa kisima cha gesi asilia unaoendelea katika Kitalu cha Songo Songo Mkoani Lindi unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa gesi asilia kwa takribani futi za ujazo milioni 20 kwa siku.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Charles Sangweni wakati wa ziara ya kikazi aliyoifanya katika kitalu hicho juzi mkoni Lindi.

Kwa mujibu wa Sangweni, ukarabati huo utagharimu takribani Dola za Marekani Milioni 20 na unatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwezi Novemba 2024.

“Ongezeko la futi za ujazo milioni 20 kwa siku unaotarajiwa mara baada ya kukamilika kwa ukarabati wa kisima hiki utakuwa na uwezo wa kuzalisha mpaka megawati 100 za umeme” alisema Sangweni.

Uzalishaji wa gesi asilia kutoka katika Kitalu cha Songo Songo ulianza mwaka 2004 kwa lengo kuu la kuzalisha umeme. 

Kwa sasa, Kitalu hicho kina jumla ya visima sita vinavyozalisha gesi asilia vikijulikana kwa SS3, SS5, SS9, SS10, SS11 na SS12.

Sangweni alisema kuwa kisima kinachofanyiwa ukarabati (SS7) kilipata changamoto ya kiufundi na hivyo kusababisha uzalishaji wa gesi asilia kutoka katika kisima hicho kusitishwa kwa muda.

Kwa robo ya kwanza ya mwaka 2024/25, uzalishaji wa gesi asilia kutoka katika Kitalu cha Songo Songo ulikuwa wa wastani wa futi za ujazo milioni 86 kwa siku.