Wanawake washauriwa kuchunguza afya zao kuepuka saratani

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 07:53 PM Oct 28 2024
Daktari Bingwa Mbobezi wa Radiolojia Tiba, Dk. Latifa Abdallah.

WATAALAMU wa masuala ya afya wametoa rai kwa wanawake na jamii kwa ujumla kuhakikisha kwamba wajiwekea utaratibu maalumu wa kwenda hospitalini na kuchunguza afya zao mara kwa mara ili kuzuia kuathiriwa na magonjwa hatari kama saratani ya matiti.

Aidha, wataalamu hao wanabainisha kuwa watu wengi wanaathiriwa na maradhi mbalimbali kutokana na kutokuwa na utaratibu huo jambo linalosababisha kufikwa na matatizo ambayo yangekuwa na uwezekano ya kuzuilika.

Akizungumza jana mkoani Dar es Salaam, Daktari Bingwa Mbobezi wa Radiolojia Tiba, Dk. Latifa Abdallah, kutoka hospitali ya Shifaa, alisisitiza kwamba ni vizuri pia kwa watu kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi kwakuwa yatasaidia kuongeza utimanu wa mwili na kuongezea uwezo kinga mwili katika kupambana na magonjwa nyemelezi.

"Leo 'jana' tumefanya matembezi ili kuonyesha 'awareness' ya saratani ya matiti na mazoezi yanatusaidia kujikinga, lakini pia ni vizuri kufanya uchunguzi wa awali mara kwa mara kwasababu saratani ya matiti ikigundulika kwenye hatua ya kwanza inatibika kwa asiliamia 100," amesema na kuongeza:

"Tafiti nyingi zimefanyika kwahiyo ni vizuri sana kujichunguza kwaajili ya kujua mapema, lakini pia hii sio kwa wanawake tuu, kuna kundi ya wanaume nao wanashangaa kwamba wanaweza kupata Saratani ya matiti, ndio utafiti umefanyika duniani na imegundulika kwamba asilimia moja ya wanaume wanapata ugonjwa huo," amesema Dk. Latifa.

Kwa mujibu wa tafiti hizo, alishauri kuwa wanaume nao ni vizuri kujichunguza kuangalia kwamba kuna kiuvimbe chochote kwenye titi au kwapa, akisisitiza kuwa endapo ataona dalili za kuwepo na uvimbe katika sehemu hizo, haraka iwezekanavyo aende kumuona daktari kwaajili ya uchunguzi wa kitaalamu.

Naye, Omary Mkangama, Mkuu wa Idara ya Utumishi na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, ambae alizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, alisema serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya kuendesha kampeni za kupambana na ugonjwa wa saratani ya matiti.

Alisema kwa upande wa serikali ziko hospitali zinazotibu ugonjwa huo ikiwemo Ocean Road, lakini hawataweza kwenda wenyewe bila kushirikiana na sekta binafsi, ndio maana wameshirikiana na hospitali zingine kama Shifaa kufanya matembezi kama sehemu ya hamasa.

"Pia katika hospitali za Kinondoni huduma za uchunguzi wa saratani kwa kina mama zinafanyika, na tunatoa rai kwa wananchi wote wajenge utaratibu wa kupima afya zao hata kwa mwaka mara mbili.

"Tunasisitiza hilo kwasababu kuna umri unapofika lazima uangalie afya yako iko katika hali gani, ma sasa hivi sekta binafsi nazo zimetoa kipaumbele katika nia ya kupambana na Saratani, hivyo tunawasisitiza wananchi Tanzania nzima kupata hamasa ya hizi kampeni zinazoendelea," alisema Mkangama.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa saratani ya matiti hutokea pale seli zilizoko kwenye matiti zinapopata kansa, na kwamba mara nyingi hutokea kwenye tezi zinazotengeneza maziwa au kwenye vifereji vinavyobeba maziwa kutoka kwenye tezi hadi kwenye chuchu.

Vile vile, inabainishwa kuwa wenye uwezekano mkubwa wa kupata maradhi hayo ni mtu mwenye umri wa zaidi ya miaka 50, aliewahi kuugua kabla, na pia kama mtu mama, dada au binti yake aliugua basi nae anauwezekano mkubwa wa kupata.

Pia wataalamu wanasema dalili awali za saratani ya matiti ni uvimbe usio na maumivu kwenye titi, na kwamba ikiwa imeenea uvimbe huwa mkubwa na huenda mtu akahisi kama ni mgumu na umekwama mahali, pamoja na ngozi iliyojuu kuwa na joto, nyekundu na wakati mwingine kuwa ngumu kama gamba.