MKUU wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amenusa ufisadi katika Chama cha Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS) Utemini, Halmashauri ya Wilaya ya Itigi katika ununuzi wa zana za kilimo, likiwamo trekta lililonunuliwa kwa Sh. milioni 65 na kuagiza ukaguzi wa hesabu ufanyike haraka.
Akizungumza jana na wananchi wa kata ya Itigi Mjini baada ya viongozi wa AMCOS hiyo kumlalamikia Ofisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, alisema ukaguzi katika ushirika huo utafanyika ndani ya siku saba kubaini kama kuna ufujaji fedha uliofanyika na wahusika watachukuliwa hatua.
"Nitaandika barua kwa DC, atatuma timu ya wakaguzi, watakagua kompyuta (laptop), mashine na trekta iliyonunuliwa kama ni bei halisi, mimi simwonei yeyote, wote ni wangu. Mnipe muda wa siku saba ukaguzi ufanyike," alisema.
Halima alisema alisema mkoa utafanya mkutano na kuongea na viongozi wa AMCOS zote mkoani Singida ili wapewe elimu ya namna ya kuendesha ushirika.
Alisema kwa mujibu wa utaratibu, vyama vya ushirika vinapaswa kufanya ununuzi wa kitu chochote baada ya kumshirikisha Ofisa Ushirika wa eneo husika na si chama kuchukua uamuzi kwenda kununua kitu chochote bila kumshirikisha.
Hatua ya Mkuu wa Mkoa wa Singida kutoa agizo la kufanyika ukaguzi katika AMCOS ya Utemini ilitokana na Mwenyekiti wa AMCOS hiyo, Geofrey Ighimbi kueleza kwamba waliamua kwenda kununua trekta bila kumshirikisha Ofisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, Daniel Sandewa kwa sababu amekuwa akiwapiga fedha kwa kuongeza bei kila wanapokwenda kununua vifaa vya ushirika.
"Mheshimiwa RC (Mkuu wa Mkoa), tunafahamu utaratibu lakini changamoto iliyopo ni Ofisa Ushirika tokea mwanzo alikuwa anatupiga katika ununuzi wa vifaa tulivyoomba, anaendelea kutupiga, tukaamua kujiengua kwake na aliposafiri kwenda Mwanza sisi tukafanya kikao tukaamua kununua trekta kwa Sh. milioni 65," alisema.
Ighimbi alisema Ofisa Ushirika huyo amekuwa 'akiwapiga' fedha kwenye ununuzi wa vifaa, mfano kompyuta mpakato (laptop) ambayo kihalisia inauzwa Sh. 300,000 lakini yeye aliwanunulia kwa Sh. milioni 1.2 na mashine ya kupepeta dengu aliwanunulia kwa Sh. milioni nne wakati bei halisi wanayojua sokoni ni Sh. milioni 1.5.
Ofisa Ushirika, Sandewa alipoulizwa na Nipashe wakati wa mkutano huo kuhusu tuhuma hizo, alisema si za kweli na kwamba amekuwa akipambana na viongozi wa AMCOS hiyo, mfano mashine ya kupepetea dengu walitaka kuuziwa kwa Sh. milioni 13, akakataa.
Alisema hata laptop waliyouziwa ni mbovu na kwamba trekta nayo wameinunua kwa Sh. milioni 81 na si milioni Sh. 65 kama walivyoeleza.
Mwanachama wa AMCOS ya Utemini, Elizabeth Ngowi, alisema viongozi wa ushirika hao wamekuwa hawatoi taarifa za mapato na matumizi ya fedha kwa wanachama na hata vifaa vilivyonunuliwa ikiwamo trekta wanachama hawakushirikishwa.
Naibu Katibu wa AMCOS, Amani Hamis, alisema si kweli kwamba wanachama hawashirikishwi katika ununuzi wa vifaa kwa kuwa hata katika ununuzi wa trekta kulifanyika kikao Oktoba 12, 2024 ambacho ndicho kilitoa uamuzi wa ununuzi wa trekta hilo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED