Mradi kuimarisha upatikanaji umeme vitongojini mbioni kuanza-Kapinga

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:00 PM Oct 31 2024
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema Serikali inatarajia kuanza mradi mpya wa upelekaji umeme vitongojini utakaohusisha ujenzi wa njia za kati na ndogo za kusafirisha umeme.

Kapinga ameyasema hayo leo Oktoba 31, 2024 bungeni jijini Dodoma  wakati akijibu swali la George Mwanisongole, Mbunge wa Mbozi aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itaanza kupeleka umeme mkubwa kwenye Vitongoji ambavyo havijapata umeme mkubwa na hivyo kukosa sifa ya kuwepo kwenye miradi ya maendeleo. 

"Kwenye mradi huu utakaoanza Desemba 2024 tumeboresha zaidi kwani tutakuwa na transfoma zenye ukubwa wa KVA 50, 100 na 200 kulingana na ukubwa wa Kitongoji." amesema Kapinga

Ameongeza kuwa, maeneo ya Vitongoji ambayo hayakunufaika na mradi wa awali wa vitongoji 15 yatanufaika kwa mradi utakaoanza Desemba 2024.

Akijibu swali la Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu aliyeuliza ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya umeme jazilishi maeneo ya Miji yenye sura za Vijiji kama Ugele, Mosi, Cargrielo, Machinjio, Ulonge, Mtalagala na Msisina, Mhe. Kapinga amesema Serikali inaendelea kupeleka umeme katika maeneo ya vijijini yakiwemo maeneo ya Miji yenye sura za Vijiji.

 Aidha, kwa maeneo ya Ugele, Mosi, Cargrielo, Machinjio, Ulonge, Mtalagala na Msisina yaliyopo katika Jimbo la Iringa Mjini, Serikali itayapelekea umeme kupitia mradi wa kupeleka umeme katika Vitongoji 15 kwa kila Jimbo.
Ameongeza kuwa, maeneo ya Cargrielo na Machinjio  yatapatiwa umeme na TANESCO kupitia miradi yake ya ndani ya kusogeza miundombinu ya umeme kwa wananchi.