WAJASIRIAMALI nchini wametakiwa kupanua wigo wa shughuli zao kwa kufanya biashara kidijitali ili kuongeza kipato na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo wakati wa kutangaza 'Mjasiriamali box' kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo kuendesha biashara zao kimtandao, Mkuu wa kitengo cha biashara wa kampuni ya Tigo, John Sicilima, alisema biashara kwa sasa zinahitaji ubunifu ili kuongeza tija na ndio sababu wengi wanashauriwa kuingia kwenye biashara kwa njia za kidijitali.
"Dunia kwa sasa inahamia kwenye kidijitali, wajasiriamali wadogo na wa kati nao lazima waende na kasi ya teknolojia, kampuni ya simu tunahimiza hivyo kwa vitendo kwa kuleta huduma itakayowasaidia kujiinua na kuchangia kukua kwa uchumi wa nchi," amesema Sicilima.
Aidha, amesema kuwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo wametoa ajira nyingi kwa watu na ndio sababu ya kuwashauri kuingia kwenye kufanya biashara kimtandao.
"Kwa sasa karibu asilimia 50 ya ajira nchini zimetoka kwa wajasiriamali, hapa nchini kuna zaidi ya wajasiriamali milioni tatu, kwa picha hii unaweza kuona namna wanavyochangia pato la taifa, kama wataingia kwenye mfumo huu wa kidijitali wataongeza zaidi mapato na kuinua biashara zao," amesema.
Mmoja wa wajasiriamali aliyeshiriki uzinduzi huo, Joshua Mwandru, Mkurugenzi wa Kampuni ya Giraffe Pharmacy Ltd, amesema kuna changamoto nyingi kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo lakini kwa sasa baadhi ya changamoto hizo zinatatuliwa kutokana na teknolijia inavyozidi kukua.
"Nimekuwa kwenye Mjasiriamali box tangu kuanzishwa kwake kwa mara ya kwanza, nimeona faida yake katika kukuza biashara, nashauri wengine waingie wataona faida yake," amesema.
Aidha, amesema kupitia huduma hiyo ameweza kuwaunganisha wafanyakazi wake wote zaidi ya 30 katika mfumo mmoja na kurahisisha kutoa huduma.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED