Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), itaendelea kujenga mazingira wezeshi na shirikishi ili kuwezesha taasisi katika sekta ya umma na binafsi kutumia masoko ya mitaji kupata fedha za kutekeleza miradi na shughuli za maendeleo.
Shughuli hizo ni pamoja na kuuza hisa kwa umma, hatifungani za miundombinu, hatifungani rafiki za mazingira, hatifungani za bluu, hatifungani za jamii na hatifungani za taasisi za serikali.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Masoko na Uchunguzi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Exaut Julius, akimwakilisha Ofisa Mtendaji Mkuu wa mamlaka hiyo, CPA Nicodemus Mkama, katika hafla ya uzinduzi wa zoezi la uuzaji wa Hisa za Upendeleo za Benki ya DCB jijini Dar es Salaam.
Julius alisema, serikali kupitia Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ina jukumu la kuendeleza na kusimamia masoko ya mitaji hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba shughuli katika masoko ya mitaji zinafanyika kwa kufuata sheria, taratibu na miongozo ili kuleta uwazi na haki kwa washiriki wote.
Kupitia uzinduzi huo Benki ya DCB inatarajia kupata zaidi ya sh bilioni 10.7 ili kuongeza kiasi cha mtaji wake unaofikia sh bilioni 15 kwa sasa, ili pamoja na mambo mengine kukidhi vigezo vilivyowekwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), pamoja na kuwaletea wanahisa wake na watanzania kwa ujumla tija za kiuchumi sambamba kuongeza mtaji wake kutoka ulipo sasa hadi kufikia sh bilioni 61 ifikapo Mwaka 2028.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya benki hiyo, Zawadia Nanyaro alisema, Uuzaji wa Hisa za upendelo unatarajia kuwaletea wanahisa na watanzania kwa ujumla tija za kiuchumi, baada ya kuongeza mtaji wa benki ambapo unalenga kukuza biashara na kuwapatia wafanyabiashara wadogo wadogo na wa kati mitaji ya kukuza biashara zao na upande mwingine umiliki wa hisa za benki ya DCB unaunga mkono juhudi zinazoendelea za serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi shupavu wa Rais, Dk Samia Suluhu Hassan za kuwaletea watu wake maendeleo.
Alisema Bodi ya Wakurugenzi ya DCB iliidhinisha mpango mkakati wa miaka mitano ukijikita kwenye mambo makuu Matano ambayo ni kukuza mtaji wa benki kutoka Sh bilioni 15 (2024) hadi kufikia shs bilioni 61 ifikapo mwaka 2028.
Alitaja jambo lingine kuwa ni ukusanyaji wa amana nafuu za benki kupitia wanahisa wakuu na wateja wao, tatu kuongeza wigo wa mikopo bora itakayotolewa kwa ufanisi na umahiri na utoaji wa mikopo kwa wateja wadogo wadogo na wa kati.
Alisema wanafanya hivyo ili kuendelea kutimiza lengo la kuanzishwa kwa benki na tano, kuboresha njia za utoaji huduma na kuongeza bidhaa zinazotolewa kwa njia za kijiditali.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED