Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imeanzisha mifuko ya uwekezaji wa pamoja, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kupanua upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi, vijijini na mijini.
Mtendaji Mkuu wa CMSA, Nicodemus Mkama, alitoa kauli hiyo katika hafla ya uzinduzi wa mpango wa uwekezaji wa kampuni ya iTrust Finance Limited, ambao unajumuisha mifuko mitano: iCash (mfuko wa soko la fedha), iGrowth (mfuko wa uwiano), iIncome (mfuko wa mgao wa mapato), iSave (mfuko wa mapato ya kudumu), na Iman (mfuko wa misingi ya shariah).
Mukama alieleza kuwa hatua hii ni sehemu ya mpango wa tatu wa huduma za fedha, wenye lengo la kuongeza ushiriki wa wananchi katika sekta rasmi ya kifedha, hasa kupitia masoko ya mitaji. CMSA iliidhinisha nyaraka muhimu na mikataba ya mifuko hiyo tarehe 11 Oktoba mwaka huu, baada ya kutimiza vigezo vya kisheria.
"Uwekezaji katika mifuko hii unaleta manufaa kwa jamii na kuchangia maendeleo ya uchumi," alisema Mukama, akiongeza kuwa mfuko huu utarahisisha upatikanaji wa rasilimali kwa miradi ya maendeleo na kuwapa wawekezaji fursa ya kupunguza vihatarishi kwa kuwekeza katika miradi mbalimbali.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED