MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amewahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuwatumia wataalamu kutoka Chuo cha Maendeleo ya Biashara (CBE) Kampasi ya Mbeya kuboresha shughuli zao.
Pia amewataka kuwatumia wataalamu wa manunuzi, ugavi na uhasibu wanaohitimu katika chuo hicho.
Alitoa ushauri huo mwishoni mwa wiki alipofanya ziara katika chuo hicho kwa lengo la kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu mipya.
Pia, aliwataka wawekezaji hao kuwatumia wataalamu wanaohtimu masomo yao chuoni hapo hasa wa ugavi na manunuzi pamoja na wahasibu.
"Nipongeze sana uongozi wa CBE kwa kuanza udahili wa masomo hayo kwa mwaka 2024, hii itakuwa chachu kubwa kwa taifa na kuwezesha kuchochea uchumi endelevu na ajira kwa vijana watakaohitimu,” alisema Homera
Homera alisema tangu kuanza kwa chuo hicho miaka 10 iliyopita huu ni mwaka wa kwanza kuanza udahili wa masomo hayo na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo kwa kuunga mkono jitihada za serikali.
Mkurugenzi wa chuo hicho, Jeremiah Wilhelm alisema uwekezaji unaofanywa na serikali kwenye chuo hicho ni kivutio kwa wananchi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuchangamkia fursa za elimu ya biashara.
Alisema ili kufikia malengo ya vijana kujiajiri chuo hicho kimewafikia wajasiriamali 600 kwa mwaka wa fedha 2022/23, kuwapatia elimu ya biashara bure kwenye mitaa, kwenye masoko na kwenye maeneo ya mikusanyiko ya vijana hasa vijiweni.
Alisema sasa hivi wameshapata mzabuni ambaye atakuwa anawauzia chakula watumishi na wanafunzi wa chuo hicho na hivyo uongeza ubora wa elimu.
Diwani Kata ya Iganzo, Daniel Mwaipopo alisema chuo hicho kimeleta mchango mkubwa wa shughuli za kiuchumi kwa jamii na wazazi kuona umuhimu wa elimu kwa vijana.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED