Serikali imethibitisha kuwa wadau wa ndani na nje ya nchi wameonesha nia ya kuwekeza katika miradi mbalimbali chini ya mpango wa BSEZ, huku mazungumzo yakiendelea na taasisi husika.
Hata hivyo, hadi sasa hakuna mwekezaji yeyote aliyeingia makubaliano rasmi na serikali, na umma utaendelea kufahamishwa kuhusu maendeleo ya utekelezaji wake.
Katika taarifa yake ya Februari 14, 2025, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema kuwa BSEZ ni sehemu ya miradi 17 ya kielelezo chini ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26). Mpango huo utahusisha ujenzi wa bandari, kongani za viwanda na Tehama, ukanda huru wa biashara, na kituo cha reli, ambapo utekelezaji wake utafanywa kupitia ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali (PPP).
Wakati huohuo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, amekanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni kuwa Tanzania imesaini mkataba wa kuipa Kampuni ya Saudi-Africa Development Company (SADC) haki ya kuendesha Bandari ya Bagamoyo. Ameeleza kuwa hakuna mkataba wowote uliosainiwa na serikali, na kwamba umma utajulishwa rasmi endapo kutakuwa na makubaliano yoyote.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Saudi (SPA), mpango wa SADC wa "East Gateway" unalenga kukuza biashara na uwekezaji Afrika Mashariki, huku Bandari ya Bagamoyo ikitajwa kuwa lango kuu la biashara kwa kanda hiyo.
Awali, mradi wa Bandari ya Bagamoyo ulianzishwa ili kupunguza msongamano wa Bandari ya Dar es Salaam na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji. Hata hivyo, ulisitishwa mwaka 2016 kutokana na vipengele vya mkataba vilivyoonekana kuwa na masharti magumu. Serikali imeendelea na juhudi za kufufua mradi huo kupitia mazungumzo na wawekezaji wa China Merchants Holdings (International) Co. Ltd (CMHI) na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman (OIA). Hadi sasa, mazungumzo yanaendelea ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa manufaa ya taifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED