Deni la bil.7/- lakwamisha ukamilishaji ujenzi wa vivuko

By Neema Emmanuel , Nipashe
Published at 11:15 AM Mar 28 2024
Mwenyekiti kamati hiyo, Selemani Kakoso.
Picha: Wizara ya Ujenzi.
Mwenyekiti kamati hiyo, Selemani Kakoso.

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeiagiza serikali kumlipa mkandarasi Songoro Marine Transport Ltd Sh.bilioni saba anazodai ili akamilishe ujenzi wa vivuko.

Akizungumza juzi baada ya kamati hiyo kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa mkandarasi huyo, Mwenyekiti kamati hiyo, Selemani Kakoso alisema wananchi wengi wa Kanda ya Ziwa wanauhitaji wa vivuko hivyo.

Hivyo, aliamuagiza Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kuhakikisha anapeleka fedha hizo kwenye huo mradi ili uweze kukamilishwa kwa wakati na kutowarudisha nyuma makandarasi wazawa katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Hapa angekuwa mkandarasi kutoka nje ya nchi lazima mgemlipa riba lakini kwa kuwa ni mkandarasi mzawa bado na yeye anahitaji kuendelea kukua ataishi kwa maumivu makali anaogopa akiwadai kwa kulazimisha mtamnyima tenda, ndicho kinachowaua wazawa" alisema Kakoso.

Baada ya maagizo hayo, Waziri Bashungwa aliahidi kufuatilia suala hilo baada ya ziara hiyo ambapo alisema ataenda kuweka kambi hazina kwa ajili ya kumuomba Waziri wa Fedha na wataalamu wake kulizingatia hitaji kubwa la mkandarasi huyo kulipwa fedha hizo ili wananchi waweze kupata huduma baada ya miradi hiyo kukamilika.

Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa kivuko kipya na maegesho ya Buyagu- Mbalika alisema  kivuko hicho chenye urefu wa mita 30.25, upana mita 9.75 kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kubeba tani 50, abiria 100 na magari madogo sita.

Alisema mpaka sasa mradi huo umefikia asilimia 45.9 na umeongezwa muda kwa miezi minne bila ongezeko la gharama kutokana na kuchelewa kwa malipo baada ya kuwasilisha hati za madai.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro Marine Transport, Meja Songoro alisema tatizo walilokutana nalo ni kuchelewa kwa malipo ambapo mpaka sasa zaidi ya Sh.bilioni Saba. 

"Katika karakana yetu ya Mwanza tunatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo Rugezi - Kisorya ambao umefikia asilimia 81, Ijinga -Kahangala asilimia 84, Bwiro - Bukondo asilimia 85, Nyakalilo- Kome asilimia 60 na Buyagu - Mbalika asilimia 45.9" alisema Songoro.