Bodi yaagizwa kuanzisha mfuko kusajili wakulima wa korosho

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 10:07 AM Apr 24 2024
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe ameiagiza Bodi ya Korosho Tanzania kuanzisha mfumo wa kusajili wakulima wa zao hilo ili kuongeza uzalishaji kutoka tani 350,000 za mwaka huu.

Bashe alitoa agizo hilo jana kwenye kikao cha tathmini ya uzalishaji, ubanguaji na masoko ya korosho kilichofanyika  jijini hapa.

Alisema lazima mfumo huo wa kusajili wakulima uwepo kwa sababu ni muhimu  kujua shughuli zao za kilimo katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema bodi hiyo ni lazima inatakiwa pia kuwa na idadi ya mikorosho, umri wa miti na wakulima wapewe namba ili waonekane kwenye orodha.

"Anzisheni mfumo wa kusajili wakulima itawasaidia pia kujua wana changamoto gani katika kilimo wanachofanya, " alisema Bashe.

Alisema lengo la serikali ni kuona zao la korosho linapiga hatua  na wakulima  kuinuka kiuchumi.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo,  Brigedia mstaafu Aloyce Mwanjire, alisema wako imara  kuhakikisha mnyororo wa thamani wa zao hilo unasonga mbele.

Brigedia Mwanjire, alisema mnyororo wa kuzalisha korosho ghafi unapaswa kuangalia kwa makini ili kuhakikisha soko la zao hilo linapatikana na wakulima wananufaika na kilimo hicho.

Aliishukuru serikali kwa usimamizi mzuri ikwenye kilimo cha korosho na kuwasaidia wakulima kupiga hatua.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweri, aliitaka bodi hiyo kufanye kazi kwa weledi ili kuhakikisha wakulima wananufaika.