Serukamba ajivunia mafanikio ya kilimo Singida

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 09:44 AM May 06 2024
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba.
Picha: Maktaba
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba.

MKUU wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba, amewaasa viongozi mkoani hapa kuweka mkazo katika matumizi ya mbolea kwenye kilimo kwa kuwa ndio njia pekee ya kuwaondoa wananchi kwenye umaskini na kuongeza uzalishaji wa mazao.

Akizungumza katika hafla ya kumuaga iliyofanyika mjini Singida juzi mjini hapa, Serukamba, alisema mwaka 2022 Singida ilitumia tani 220 za mbolea na  kiwango kikaongezeka na kufikia tani 6,400 mwaka jana  jambo ambalo  kama mkuu wa mkoa huo kwa vipindi hivyo  aliona amefanikiwa kwa kiwango kikubwa.

Alisema ameshangaa baada ya kuhamishiwa Iringa amekuta mwaka jana katika mkoa huo, walitumia tani 36,000 za mbolea kati ya lengo ka kutumia tani 42,000.

"Nikuombe dada yangu Halima (Halima Dendego) Mkuu wa Mkoa wa Singida hili la mbolea lipe fursa ndio 'game change' ya maendeleo ya watu wa Singida," alisema Serukamba.

Alisema bahati nzuri ni kwamba serikali imeweka fedha kwenye mbolea ili watu waweze kununua kwa bei ambayo ni nusu, hivyo hakuna sababu ya kutowafanya wakulima wasitumie mbolea kwenye kilimo.

Naye Dendego, alimshukru Serukamba kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kusimamia maendeleo wakati akiwa Singida kwani kila sehemu ameacha alama.

 "Nimeshamaliza wilaya zote, nimepita halmashauri zote nimekuta alama yako kila ninapokanyaga, umefanya kazi kubwa sana, umesukuma sana miradi na mimi naungana na wanasingida pale pale ulipoachia kaka yangu ili tusonge mbele," alisema.

 "Yeye (Serukamba) ni baba mimi ni mama tunaweze tusifanane katika staili ya uongozi, lakini tutafanana katika malengo ya mafanikio, ukiona tunasukumana ndugu zangu ni katika kazi nje ya hapo ukitimiza wajibu wako mimi ni dada, mimi ni mama na mimi ni rafiki, sina historia ya kugombana na mtu," alisema.