UNAPOZURU wilayani Chunya mkoani Mbeya, kuna mchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu katika halmashauri ya wilaya hiyo, kazi yake mpya inatoa ajira kwa vijana zaidi ya 100.
Waajiri hao ni kutoka mikoa mbalimbali, huku akitoa mapendekezo kwa serikali namna ya kuongeza tija ya uzalishaji ikiwamo, kuondoa changamoto zilizopo kwa wachimbaji.
Hiyo inatokea, huku sekta ya madini ikiwa moja ya vyanzo muhimu vinavyoingizia mapato makubwa umma, huku serikali nayo ikitegemea mapato kutokana na tozo za kodi kutoka katika sekta hiyo.
Wakati serikali ikiweka mikakati yake kuongeza mapato na kuingiza maboresho kwa wachimbaji, inayojumuisha kuwapatia mikopo, pamoja na maeneo sahihi ya uchimbaji, kuna utata unajitokeza katika mchakato kamili wa kufanikisha kazi hiyo.
Hiyo inatajwa kwa sasa inawafanya wengi wamekuwa wakichimba kwenye maeneo yenye leseni za watu licha ya kuwa maeneo hayo hawayatumii.
Akizungumza na Nipashe, mbunifu Khamis Rajab Salum, ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni yake, anasema alikuwa mjasiriamali anayefanya kazi ya kuchomelea vyuma, baadae akajiingiza kwenye uchimbaji madini, alikotumikia kwa miaka saba, hata kufanikiwa kuajiri vijana zaidi ya 100 wa kada mbalimbali, mgongo wa kampuni yake.
Anasema, hadi sasa anamiliki migodi mitatu ya kisasa, ikiwa ngazi ya juu zilizoko wilayani Songwe na mbili, huko Makongolosi, Chunya, huku akiwa na mtambo mkubwa maarufu ‘karasha’ za usaga mawe tani tatu na nusu kwa saa.
Salum anasema, katika jitihada zake anamiliki malori manne, vilevile trekta, mitungi na mitambo ya kuchoma umeme.
Anajigamba ni hali inayomfanya kulipa kodi na mishahara ya wafanyakazi wake kwa wakati, huku akishiriki kikamilifu kwenye shughuli za kijamii katika maeneo na nje ya miradi wake.
Salum anaeleza sehemu ya faida anayopata amekuwa akitoa misaada kwa watoto yatima kwenye vituo vilivyopo mkoani Mbeya, akirejea mfano wa hivi karibuni amechangia mifuko 100 ya saruji yenye thamani ya shilingi milioni 2.1 kwenye ujenzi wa Kituo cha Afya Makongolosi.
Pia anasema, michango anaielekeza kwenye nyumba za ibada, wazee wasiojiweza jijini Mbeya na kwenye ujenzi wa shule ya sekondari, akinena nako katoa mifuko 100 ya saruji.
MAONI YAKE KISERIKALI
Mchimbaji huyo mdogo, anaitaja sekta hiyo ya madini ni muhimu na inachangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa, hivyo ili mafanikio makubwa zaidi yapatikane, serikali kupitia Wizara ya Madini, iwape maeneo maalum ya kuchimba wachimbaji wadogo na kuwapatia mikopo.
Anasema, wachimbaji wadogo wengi hawana migodi, wengi wao zaidi ya 200 walikuwa wakichimba kwenye eneo linalojulikana kwa jina la ‘Gepu’ lakini akajitokeza mtu aliyewafukuza akidai eneo hilo ni lake na amepewa leseni.
Kufukuzwa kwa wachimbaji hao, anakutaja kumewapa magumu anaowataja kuwa ‘wachimbaji wenzake’, kwamba wamehamia kwenye eneo lake kufanya kazi yao.
Anasema, hadi sasa kuna maeneo (makarasha) zaidi ya 14 yamefungwa na kila moja linakuwa na wachimbaji kati ya 10 hadi 12 wanaofanya kazi hapo.
‘’Wachimbaji hawa wamefukuzwa kwenye eneo lile la ‘gepu’, wamekuja kuchimba kwenye eneo langu na wamefunga makarasha.
“Siwezi kuwafukuza kwa kuwa wanatafuta riziki ila inatakiwa serikali itafute eneo lingine lisilotumika kuwahamishia wachimbaji hawa ili kuepuka kutofanyika kwa mambo mabaya ikiwaemo wizi,’’anasema.
Khamis anashauri serikali kutambua kuwa wachimbaji wasio na maeneo, ndio wazalishaji wakubwa wa dhahabu nchini, kwani wanapoingia kujipatia riziki, huongeza wingi wa dhahabu kitaifa kwa ujumla.
Anaongeza kuwa, hata Ofisi ya Madini mkoani humo imeshamtunuku tuzo mara nyingi.
MCHIMBAJI ALIYEUIBUKA
Zebedayo Mumusi, ambaye ni mchimbaji mdogo, anasema hali ya kuwapo vitalu vya uchimbaji ambavyo wenyewe hawafahamiki, umekuwa ukiwakwaza wengi.
Hapo anafafanua: “Tunasikia kuwa kuna vitalu vimepatikana, lakini serikali inapaswa kutangaza au kuitisha mkutano kwenye maeneo husika, ili kila mmoja asikie na kama atapenda kupata eneo lake basi iwe ni suala la kuomba lakini wakiwa wame fahamishwa.”
Anaendelea kushauri kuwa serikali kwa kutumia mbinu ya kusaidia vijana wasiomudu gharama, wapatiwe kama vikundi, ili kuwawezesha kuzalisha dhahabu, bidhaa yenye nafasi kubwa katika pato la taifa.
Mumusi anasema kuwa, elimu zaidi kwa wachimbaji ifanyike ikiwamo ya kisheria, kwani migogoro imekuwa ikijitokeza ya wachimbaji na wenye maeneo, sehemu nyingi zikiwa zimetelekezwa na serikali inakosa mapato.
Hapo anamaanisha dhana ya elimu kwa wauzaji baruti, ifanyike kwa wanaoziuza kienyeji.
Mchimbaji mkongwe, George Kasanda, ambaye kwa sasa anamiliki mgodi na akiwa na wafanyakazi zaidi ya 50, anatumia uchimbaji wa mashine zaidi.
Anataja wakati Waziri wa Madini, anamtaja Profesa Sospeter Muhongo, anamsifu kuwatetea sana wachimbaji wadogo.
Anasema zama za miaka 2010, kukiwapo Waziri huyo, binafsi ana kumbukumbu jinsi wachimbaji wadogo walivyoshiriki kuandaa Sera ya Madini, akiwamo yeye mwenyewe.
Anasema, ili kuondoa migogoro kati ya wataalamu wa wakulima na wachimbaji, ni muhimu wakaletwa waaalamu madini na wahusika wengine kutoa elimu ya uhalisia na mipaka iliyoko kwenye maeneo hayo ya uchimbaji, kilimo na makazi.
Kasanda anashauri hapo kuwa, maeneo yenye mikondo ya madini, hayafai kuwe makazi ya watu na wanapaswa kuandaa ramani husika, serikali ikiruhusu watafiti binafsi, ili kuongeza ushindani unaikuza sekta hiyo.
Aidha, Kasanda anashauri kuwa serikali itafute mitambo ya utafiti na ikiwezekana iwakodishie wachimbaji wadogo, ili kuendana na teknolojia ya kisasa.
Hadi sasa anataka wachimbaji wengi wanatumia nyenzo za kizamani, inayochelewesha upatikanaji dhahabu kwa wingi.
UONGOZI WILAYA
Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa Mbeya, Laurent Mayala, anasema serikali imejipanga kuhakikisha wachimbaji wanaondolewa changamoto zao ikiwa.
Hapo anataja kujumuisha kupatiwa maeneo ambapo tayari zaidi ya vitalu vyenye leseni 1500 vilivyokuwa havitumiki, huku mambo mengine yakiendelea kutatuliwa.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbaraka Batenga, anasema kutokana na sekta hiyo ya madini kuwa umuhimu, serikali imejipanga kuwaongezea tija wachimbaji na kuweka lengo la kukusanya kilo 500 kila mwezi.
Katika hilo anataka kufanikishwa vitalu vyenye leseni 1505 vilivyokuwa havitumiki vimechukuliwa na kupewa wachimbaji wadogo kwa kuanzia.
Mkuu wa Wilaya anasema,uongozi wake unaendelea kuzishawishi benki ziwakopesha wachimbaji wadogo, kwa ajili ya kufanikisha shughuli za uchimbaji.
Anakiri kutambua umuhimu wa wachimbaji wadogo, akisema kuwa ‘ni benki ikawaamini.’
Pia, Batenga anasema hakuna mchimbaji mwenye lesseni amelalamika kushindwa kurudisha deni, hivyo ana matumaini hata benki hizo zikiwakopesha, deni kulipwa kwa mujibu wa makubaliano.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED