WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amekemea vitendo vya ubabaishaji na rushwa miongoni mwa watumishi wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) akisema vinaweza kufuta mazuri yote ambayo taasisi hiyo imeyafanya na inayoendelea kuyafanya.
Akizungumza na menejimenti ya TEMESA na mameneja wa Mikoa jijini Dodoma leo Waziri Ulega ameeleza kuwa serikali imedhamiria kuifanya wakala hiyo kuwa taasisi namba moja na kimbilio la wote katika utengenezaji wa magari ya serikali na binafsi.
Amesisitiza kuwa wanatakiwa kupiga vita vitendo vya ubabaishaji na rushwa. Akieleza kuwa huo ndiyo ugonjwa unaoharibu taasisi nyingi hivyo wanatakiwa kutumia uwezo wao wote kupambana na jambo hilo.
"Pia hongereni kwa kuanzisha mkakati mpya wa kufanya kazi utakaowawezesha kujiendesha kibiashara kwa kushirikiana na sekta binafsi pale inapobidi ili kuihudumia jamii kikamilifu. Sisi TEMESA ni lazima tuwaoneshe watu ukinilipa nitakufanyia kazi kwa wakati," amesema Ulega.
Ameongeza kwa kuzisisitiza taasisi zingine za serikali zinazopatiwa huduma na wakala hiyo, kuweka mikakati ya kulipa madeni yao kwa wakati ili kuisaidia TEMESA kuondokana na madeni.
Aidha, ameeleza kuwa zaidi ya Sh. Bilioni 67.4 zimetumika katika miaka mitatu ya serikali chini ya Samia Suluhu Hassan kujenga vivuko vipya sita, ukarabati wa vivuko saba na ujenzi wa miundombinu ya vivuko ambayo ni maegesho na majengo ya abiria katika Ziwa Victoria na Bahari ya Hindi.
Hata hovyo, kiongozi huyo amepongeza ukarabati wa karakana za matengenezo ya magari unaoendelea kufanyika kote nchini na kusisitiza ukarabati huo uendane na mabadiliko ya kimtazamo, utaalamu na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ili kuleta tija na ufanisi katika majukumu yao.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED