AMCOS yamchangia mbunge Sh.120,000/- achukue fomu Uchaguzi Mkuu 2025

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 07:37 PM Dec 20 2024
AMCOS yamchangia mbunge  Sh.120,000/- achukue fomu Uchaguzi Mkuu 2025.
Picha: Shaban Njia
AMCOS yamchangia mbunge Sh.120,000/- achukue fomu Uchaguzi Mkuu 2025.

Chama cha Ushirika cha Msingi (AMCOS) kilichopo Kata ya Ulowa, Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga, kinachojihusisha na kilimo cha tumbaku, kimemkabidhi kiasi cha Shilingi 120,000 Mbunge wa Ushetu, Emmanuel Cherehani, kwa ajili ya kuchukua fomu ya kugombea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Hatua hiyo inalenga kuthamini juhudi zake za kuhakikisha pembejeo za kilimo zinapatikana kwa wakati.

Mwenyekiti wa chama hicho, Costantina Maganga, alikabidhi fedha hizo jana mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Ushetu, uliofanyika katika Kata ya Ukune na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita.

Maganga alisema kuwa walichukua hatua hiyo kutokana na juhudi za Mbunge Cherehani za kuwakilisha masuala ya wakulima wa tumbaku bungeni. Alisema mbunge huyo amekuwa akihakikisha pembejeo na mbolea zinapatikana kwa wakati pamoja na masoko ya uhakika. Fedha wanazopata kutoka kwenye zao hilo zimewasaidia kuboresha maisha yao, na walitaka fedha hizo zitumike kwa ajili ya kuchukulia fomu ya kugombea ubunge mwaka 2025.

Pia, Maganga aliwaahidi viongozi wa serikali kuwa hawatoruhusu tumbaku kutoroshwa na kwamba wataendelea kuuza tumbaku kwenye masoko yanayotengwa na serikali ili kuhakikisha Halmashauri ya Ushetu inapata mapato yake. Alisisitiza kuwa watawafichua na kudhibiti wale wote watakaotorosha tumbaku.

Mbunge wa Ushetu, Emmanuel Cherehani, alipokea fedha hizo kwa shukrani kubwa. Aliahidi kuzitumia kama ilivyopangwa kwa ajili ya kuchukulia fomu ya kugombea. Aidha, alisisitiza dhamira yake ya kuendelea kuwahudumia wananchi kwa kuhakikisha maendeleo katika sekta za afya, kilimo, maji, na miundombinu ya barabara yanafanikiwa.

Mbunge huyo alieleza kuwa kati ya mwaka wa fedha 2021 hadi 2024, jimbo hilo lilipokea Shilingi bilioni 190 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali. Alisema kuwa hospitali ya wilaya sasa imekamilika, na wananchi wanapata huduma za afya karibu na makazi yao tofauti na hapo awali walipokuwa wakisafiri kwenda Hospitali ya Manispaa ya Kahama.