SHUWASA kutumia milioni 338 kupanua mtambo wa kuchakata tope kinyesi

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 02:40 PM Dec 20 2024
Gari la majitaka.
Picha: Mtandao
Gari la majitaka.

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) ipo katika hatua za utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa mtambo wa kuchakata tope la kinyesi uliopo Kata ya Kizumbi, Manispaa ya Shinyanga.

Mradi huo unalenga kuboresha huduma za usafi wa mazingira kwa wananchi wa eneo hilo.

Meneja wa Uendeshaji wa Miundombinu wa SHUWASA, Mhandisi Wilfred Lameck, alieleza kuwa lengo la mradi ni kuongeza uwezo wa mtambo ili kukidhi mahitaji ya wakazi wa Shinyanga. 

Alisema awali, mtambo ulikuwa na uwezo wa kuchakata mita za ujazo 40 za tope la kinyesi kwa siku, lakini baada ya upanuzi uwezo utaongezeka hadi mita za ujazo 100 kwa siku. Hadi sasa, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 62, ukiwa na gharama ya shilingi milioni 338.

Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola, alisema mtambo huo ulianzishwa kwa ushirikiano kati ya SHUWASA, Shirika la Maendeleo la Uholanzi (SNV), na Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga. Mtambo unalenga kuchakata tope la kinyesi kutoka majumbani pekee, na utafaidisha takriban wakazi 200,000 wa Manispaa ya Shinyanga na maeneo ya jirani.

Aidha, Mhandisi Katopola alimhimiza mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha anaukamilisha kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa ili thamani ya fedha iweze kuonekana. Kwa upande wake, Mkandarasi Swalehe Maganga wa Kampuni ya Kanuta Engineering Supply alihakikishia kwamba mradi huo utakamilika ndani ya muda uliopangwa kulingana na mkataba.

Mradi huo unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika usafi wa mazingira na afya ya umma kwa wakazi wa Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya jitihada za SHUWASA za kuboresha huduma za msingi kwa wananchi.