UMOJA wa Benki Tanzania (TBA) imesisitiza kutolewa kipaumbele juu ya matumizi ya teknolojia ya kidijiti, kama njia kuu ya kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 katika ukuaji wa uchumi.
Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa mkutano wa taasisi za kifedha na Tume ya Mipango kuhusu uhakiki wa rasimu ya dira ya maendeleo, Mkurugenzi Mtendaji TBA Tuse Joune, ameeleza kwamba teknolojia inaweza kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii kwa taifa.
“Tanzania imeweka msingi madhubuti na mifano halisi katika sekta ya kifedha, mawasiliano ya simu, afya, na usafirishaji. Tunapaswa kuwekeza vya kutosha na kwa kimkakati katika eneo hili ili kupata manufaa halisi,” amesema Tuse.
Ametoa mfano wa jinsi sekta ya benki imekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha huduma za kidijiti kwa kushirikiana na sekta ya mawasiliano, akibainisha kuwa uchumi wenye nguvu unahitaji sekta ya kifedha inayotumia teknolojia kusaidia ukuaji wa sekta nyingine.
“Maendeleo ya kiteknolojia katika utoaji wa huduma za kibenki yanaonesha kuwa sekta ya kifedha tayari ina msingi thabiti wa matumizi ya teknolojia na sayansi. Teknolojia inatoa suluhisho la changamoto za uzalishaji, kuongeza thamani, na usambazaji wa bidhaa, huku ikiimarisha uwezo wa ukuaji wa sekta za kiuchumi na kijamii nchini Tanzania,” amesema Tuse.
Ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia katika sekta ya kifedha si muhimu tu kwa kuboresha huduma za kifedha bali pia kwa kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya kifedha na sekta nyingine zenye kipaumbele katika Dira ya 2050.
Pia Tuse ametaja maeneo kadhaa yanayohitaji kuimarishwa katika Rasimu ya Dira ya Maendeleo 2050, ikiwamo eneo la ufadhili wa ubunifu.
“Tunapendekeza kuwa sehemu hii iongeze umuhimu wa taasisi za kifedha za maendeleo kama vile TIB, TADB, na TMRC. Taasisi hizi zinapaswa kupata msaada wa serikali ili ziweze kutoa ufadhili wa muda mrefu kwa miradi mikubwa,” amesema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED