Familia moja imenusurika kifo baada ya kupata ajali katika eneo la Kizumbi, Manispaa ya Shinyanga.
Ajali hiyo ilitokea leo majira ya saa 9 mchana, wakati gari aina ya Harrier, lenye namba za usajili T.223 DQR, likivutwa na gari aina ya Noah, lenye namba za usajili T.885 CQG. Gari hilo liliteleza baada ya bomba la kuvutia gari kukatika, na hatimaye kutumbukia mtaroni.
Mmoja wa wanafamilia hao, Diana Wilbert, ameeleza kwa waandishi wa habari kuwa walikuwa wakitoka Dar es Salaam. Walipofika eneo la Tinde, wilayani Shinyanga, gari yao iliharibika. Walilazimika kutafuta gari lingine kwa ajili ya kuivuta hadi Shinyanga Mjini kufanyiwa matengenezo.
“Tulipofika maeneo ya Kizumbi, bomba lililokuwa likitumika kuvuta gari yetu lilikatika, na magari yote mawili yalianguka. Tunamshukuru Mungu hakuna aliyeumia vibaya zaidi ya michubuko midogo. Sote tupo salama,” amesema Diana.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa hakukuwa na kifo chochote. Amebainisha kuwa chanzo cha ajali kilikuwa kukatika kwa cheni iliyotumika kuvutania magari hayo, hali iliyopelekea magari hayo kuanguka.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED