Stendi ya Lundusi kuinua uchumi wa wananchi wa Ruvuma

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 03:05 PM Dec 20 2024
news
PICHA: FAUSTINE FELICIANE
Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Manispaa ya Songea, Hosana Ngunge (kushoto) akikagua matofari yanayotumika kwenye ujenzi wa stendi ya mabasi katika kijiji cha Lundusi kata ya Peramiho mkoani Ruvuma.

Kukamilika kwa stendi ya mabasi katika kijiji cha Lundusi, Kata ya Peramiho, Wilaya ya Songea, Mkoa wa Ruvuma, kunatarajiwa kuchangia pakubwa katika kuinua uchumi wa wananchi wa kijiji hicho na maeneo ya jirani.

Mradi huo unatekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa lengo la kuwasaidia wananchi kuepukana na changamoto za usafiri.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa ujenzi huo, Mtendaji wa Kijiji cha Lundusi, Imelda Mbawa, alisema stendi hiyo itapunguza gharama na usumbufu kwa wananchi ambao kwa sasa wanalazimika kusafiri kwenda Songea mjini ili kupata huduma ya usafiri wa mabasi.

“Kwa sasa, tunatumia gharama kubwa. Kwa mfano, mtu anayetaka kusafiri kwenda Dar es Salaam, Iringa, au Mbeya lazima aende Songea mjini na mara nyingine kulazimika kulala huko ili kesho yake apande basi. Stendi hii ikikamilika, changamoto hiyo itakuwa historia,” alisema Mbawa.

Henrik Haule, mjumbe wa kamati ya ujenzi wa stendi hiyo, aliongeza kuwa mradi huo utatoa fursa za kiuchumi kwa wananchi, hususani vijana na akina mama, kwa kuwawezesha kufanya biashara na kuongeza kipato.

“Tunaishukuru sana TASAF kwa kutuletea mradi huu. Tunaamini kwamba uchumi wa wananchi utaimarika kupitia fursa za biashara, na kijiji kitapata mapato kupitia ushuru na kodi mbalimbali,” alisema Haule.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Songea, Hassan Mtamba, alieleza kuwa stendi hiyo itarahisisha sana huduma za usafiri kwa wakazi wa Lundusi na vijiji vya jirani. Aliongeza kuwa mabasi makubwa kutoka maeneo mbalimbali yatakuwa yakifika moja kwa moja Lundusi, hatua itakayopunguza gharama na usumbufu kwa wananchi.

1

“Serikali kupitia TASAF imeonyesha dhamira ya dhati ya kusaidia wananchi. Tunaishukuru sana kwa mradi huu ambao unaenda kubadilisha maisha ya wakazi wa Lundusi na maeneo jirani,” alisema Mtamba.

Fundi kiongozi wa ujenzi huo, Peter Mashine, alibainisha kuwa mradi huo umefikia asilimia 78 na unatarajiwa kukamilika Januari mwaka ujao.

“Ujenzi huu ulianza Agosti 2023, na stendi itakuwa na sehemu ya kupaki mabasi, vyumba 36 vya biashara, matundu nane ya vyoo, jengo la utawala, na jengo la ulinzi na usalama. Tumetumia wazabuni wa ndani wa Wilaya ya Songea kwa vifaa vya ujenzi ili kuimarisha uchumi wa eneo hili,” alisema Mashine.

Mratibu wa TASAF katika Manispaa ya Songea, Hosana Ngunge, alisema utekelezaji wa mradi huo ulitokana na maombi ya wananchi wa kijiji hicho. Alifafanua kuwa asilimia 10 ya nguvu kazi ya ujenzi huo inatolewa na wananchi wa Lundusi, hatua inayolenga kuwawezesha pia kijamii na kiuchumi.

“Tunaamini kuwa stendi hii itachochea ukuaji wa uchumi wa kijiji na wananchi wake baada ya kukamilika Januari mwakani,” alisema Ngunge.

Mradi wa stendi ya mabasi ya Lundusi unatarajiwa kuboresha si tu huduma za usafiri, bali pia kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika kijiji hicho na maeneo ya jirani.

2