Watumishi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) wametakiwa kuzingatia weledi katika kutekeleza jukumu lao la msingi la kusimamia usalama na afya mahali pa kazi ili kuwahakikishia wananchi upatikanaji wa huduma bora.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mary Maganga, alipokuwa akifunga Kikao cha Tatu cha Baraza la Tano la Wafanyakazi wa OSHA kilichohitimishwa jana (Desemba 19, 2024) Jijini Arusha.
Akiwasilisha hotuba yake ya kufunga kikao tajwa, Katibu Mkuu, Mary Maganga, amesema kwakuzingatia wajibu wa OSHA wa kuzuia ajali, magonjwa na vifo mahali pa kazi, utekelezaji wa majukumu husika unahitaji weledi wa hali ya juu.
“Nitumie fursa hii kuwakumbusha kutekeleza majukumu yenu kwa kuzingatia weledi,kuwa na nidhamu na kuepuka visingizio vya aina yoyote katika kutekeleza majukumu yenu ya kila siku. Tukifanya kazi kwa weledi, tutaepuka kuwasababishia machungu zaidi wananchi tunaowahudumia ambao wakati mwignine wanakuwa wamekumbwa na matatizo kama vile ajali mahali pa kazi, kupoteza wapendwa wao au kuharibiwa malizao,” amesema Katibu Mkuu.
Aidha, amewataka viongozi wa TUGHE na vyama vingine vya wafanyakazi kufanya jitihada kuzuia migogoro baina ya waajiri na wafanyakazi mahali pa kazi badala ya kusubiri kutatua migogoro inayotokea.
Awali, akimkaribisha Katibu Mkuu kufunga kikao, Mtendaji Mkuu wa OSHA,Khadija Mwenda, amesema kikao cha Tatu cha Baraza la Wafanyakazi wa OSHA kilikuwa maalum kwa ajili ya kutathmini utendaji wa Taasisi kwa mwaka 2023/2024 pamoja na robo ya kwanza ya mwaka 2024/2025.
“Kwa mujibu wa taarifa ya Taasisi yetu ya mwaka fedha 2023/2024 na robo ya mwaka 2024/2025, tumefanikiwa kutimiza na hata kuvuka baadhi ya malengo yaliyopangwa na baraza hili jambo linaloashiria kwamba tunaenda vizuri,” amesema Mwenda.
Kwa upande wao Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Mudathir Athuman na mwakilishi wa wafanyakazi wa OSHA, Alfredy Shechambo, wameipongeza Menejimenti ya OSHA kwa kuandaa vikao vya
mabaraza ya wafanyakazi kwa mujibu wa sheria za nchi pamoja na kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi yenye lengo la kuimarisha utendaji wao.
Mabazara ya Wafanyakazi nchini yapo kwa mujibu wa Waraka wa Rais Namba 1 wa mwaka 1970 uliowaelekeza waajiri kuwashirikisha wafanyakazi mahali pa kazi katika kupanga, kutekeleza na kutathimini matokeo ya kazi zinazofanyika.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED