Viongozi wa dini mkoani Tanga wameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kujenga mahusiano mazuri na walipa kodi ili kupunguza migogoro na changamoto za kufuatilia ulipaji wa kodi.
Ushauri huo umetolewa wakati wa kikao cha kufunga Juma la Shukrani kwa Wateja lililoandaliwa na TRA, ambacho kiliwaleta pamoja viongozi wa dini na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu ulipaji wa kodi.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Askofu wa Kanisa la Moravian Tanzania, Lazaro, ameishauri TRA kuangalia kwa upya ulipaji wa kodi na taasisi za dini, huku akitoa wito wa kushughulikia magari yaliyohifadhiwa kwa muda mrefu kwenye maegesho bila kutumika.
Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Thomas Masese, amesema mamlaka hiyo inaendelea kufanya juhudi kubwa za kuimarisha mahusiano na walipa kodi kwa kuwakaribia zaidi. Alibainisha kuwa katika Juma la Shukrani, TRA imetoa zawadi mbalimbali kwa walipa kodi wanaozingatia muda wa kulipa.
Ameongeza kuwa hatua hiyo inalenga kuwahamasisha walipa kodi wengine kutimiza wajibu wao kwa hiari na kuepusha migogoro isiyo ya lazima.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED