Ujenzi mradi wa JNHPP mbioni kukamilika

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:07 PM Dec 20 2024
Ujenzi mradi wa JNHPP  mbioni kukamilika.
Picha:Mpigapicha Wetu
Ujenzi mradi wa JNHPP mbioni kukamilika.

Uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) jana Desemba 19, 2024 ulitembelea Mradi wa Kufua umeme wa Bwawa la Julius Nyerere kujionea kasi ya maendeleo ya ujenzi na kuweka mkazo wa wasimamizi kuhakikisha usimikaji wa mashine nne zilizobakia unafanyika ipasavyo ili umeme utakapozalishwa uingizwe kwenye Gridi ya Taifa kwa mafanikio yatakayoleta tija inayotarajiwa kwa watumiaji wa umeme.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Mha. Gissima Nyamo-Hanga alisema kwasasa jumla ya mashine tano (05) zimekamilika kwa asilimia 100 yaani mashine namba 9, 8, 7, 6 na 5 na tayari zimeanza uzalishaji wa umeme. 

" Tumetembelea mradi huu kujionea shughuli zinazoendelea na kuweka msisitizo wa usimamizi bora kwa maeneo ambayo bado hayajakamilika ambapo utekelezaji kwa ujumla umefikia asilimia 99.55 huku shughuli za uzalishaji wa umeme zikiwa zimeanza na wastani wa megawati 1175 zinazozalishwa  kutoka mashine tano za mradi huu zimeingizwa kwenye grid ya Taifa " alieleza Mha. Gissima. 

 Alibainisha kuwa utekelezaji wa usimikaji wa mashine namba 4 umefikia asilimia 100 ambapo kwasasa mashine hiyo ipo kwenye majaribio huku mashine namba 3 ikiwa kwenye asilimia zaidi ya 87 za usimikwaji, asilimia ambazo zinadhihirisha kuwa kiwango cha utendaji kazi ni kizuri .

Aliwahimiza wasimamizi wa mradi kuhakikisha wanaendeleza bidii  kusimamia maeneo ambayo bado hayajakamilika kuhakikisha kazi inafanyika kwa viwango vilivyoainishwa wakati wa usanifu wa mradi huo.

" Niwaombe msimamie vizuri kuhakikisha ufanyaji kazi wa mashine unakuwa ni mzuri ili umeme unaoendelea kuzalishwa unapoungwa kwenye Gridi ya Taifa usilete changamoto yoyote " alisisitiza Mha. Gissima. 

Katika hatua nyingine,  Mha. Gissima aliishukuru , Serikali  pamoja na Wizara ya Nishati na viongozi wake wote kwa namna ambavyo mara zote imeunga mkono kwa kutoa fedha na ushirikiano katika kusimamia utekelezaji wa mradi mpaka kufikia hatua iliyopo sasa pamoja na miradi mingine mingi inayoendelea nchini .

" Ninawaahidi watanzania wenzangu kuwa,  sisi kama  viongozi wa TANESCO tutahakikisha tunasimamia mradi huu kwa dhati na umadhubuti mkubwa ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kuleta tija ya kiuchumi na kijamii katika taifa letu la Tanzania" alihitimisha Mha. Gissima.

Mradi wa  Kufua Umeme wa Julius Nyerere tayari umeanza kuleta matumaini makubwa ya Kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme nchini ikiwa ni kati ya Juhudi kubwa za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt Samia Suluhu Hassan.