Wasimamishwa kazi madai kifo mama aliyeng’atwa na nyoka kukosa matibabu

By Jaliwason Jasson , Nipashe
Published at 10:32 AM Dec 20 2024
Kituo cha Afya cha Magugu, Babati mkoani Manyara.
Picha:Mtandao
Kituo cha Afya cha Magugu, Babati mkoani Manyara.

SAKATA la mgonjwa Juliana Obedi (43) aliyeng’atwa na nyoka kufia katika Kituo cha Afya cha Magugu, Babati mkoani Manyara, limewang’oa kwenye ajira watu watatu wanaodaiwa kumcheleweshea matibabu kwa saa sita, wakitaka kulipwa kwanza Sh. 150,000.

Tayari serikali imetangaza kuanza uchunguzi kuhusiana na tukio hilo kwa ushirikiano wa timu ya wataalam wa halmashauri, mkoa na mabaraza ya kitaaluma. 

Taarifa iliyotolewa kwa umma jana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Benedict Ntabagi, iliwataja waliosimamishwa kazi kupisha uchunguzi ni watoa huduma watatu wa Kituo cha Afya Magugu, ambao ni ofisa tabibu, ofisa muuguzi msaidizi na mteknolojia wa dawa.

 Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Desemba 18, mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji amefikia uamuzi huo ili kupisha uchunguzi wa tukio hilo kutokana na watumishi hao kutuhumiwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo. 

"Pamoja na changamoto iliyojitokeza ya mgonjwa huyo kucheleweshwa huduma katika kituo cha afya kwa saa sita baada ya kung'atwa na nyoka, mkono wa kulia aliong'atwa ukiwa umevimba na kubadilika rangi, vinaashiria tayari sumu ilikuwa imemwathiri sana mama huyo," ilieleza taarifa hiyo.  

Vilevile, taarifa ilieleza kuwa wataalamu hao wa afya, walipaswa kumpatia huduma stahiki zote kwanza mgonjwa kwa dharura na masuala ya malipo yangekamilishwa baadaye. 

Taarifa hiyo ilieleza zaidi kwamba kwa mujibu wa Sera ya Afya ya Mwaka 2007 na miongozo yake makundi maalumu yakiwamo ya wajawazito, watoto chini ya miaka mitano na wazee wasiojiweza wanatakiwa kupatiwa matibabu bure. 

Aidha, zinapohitajika huduma za dharura, mgonjwa anatakiwa kuhudumiwa na kama hayumo kwenye kundi la msamaha, basi taratibu za malipo zifuate baada ya kukamilisha huduma. 

Kwa  muktadha huo, taarifa ilisema  uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kufanyika kwa ushirikiano wa timu ya wataalamu wa halmashauri, mkoa na mabaraza ya kitaaluma na hatua zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kuwa na hatia katika tukio hilo.

 Pia taarifa ilisema halmashauri inaendelea kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya na kuitaka jamii mara wanapopata dharura ya kiafya zinazohitaji matibabu ya haraka kuwahi kwenye vituo vya kutolea huduma mapema bila kuchelewa.