KATIKA sehemu ya tatu ya ripoti hii jana, kulikuwa na ushuhuda wa miundombinu chakavu shuleni Lipumba, wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma. Endelea na sehemu ya mwisho kupata undani wa mustakabali wake.
HAKUNA utafiti rasmi uliofanyika shuleni Lipumba kubaini madhara ya madarasa kujengwa karibu na makaburi na athari za uhaba na uchakavu wa miundombinu shuleni huko.
Hata hivyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, katika ripoti yake ya mwaka 2020/21, anabainisha kuwa uhaba na uchakavu wa miundombinu shuleni ni miongoni mwa sababu zinazochangia ufaulu duni wa wanafunzi wa shule za msingi nchini.
Ufuatiliaji wa mwandishi wa habari hii kuhusu mwenendo
wa kitaaluma shuleni Lipumba, umebaini shule hiyo haifanyi vizuri kitaaluma.
Matokeo ya mitihani ya taifa, ambayo kitaaluma na kiserikali ndio nyenzo halisi ya kufanya tathmini kilichovunwa katika uwekezaji huo, yanaonesha shule hii ina tatizo.
Kwa mujibu wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), kwa miaka minne kuanzia mwaka 2021 hadi 2024, hakuna mwanafunzi kutoka Lipumba aliyefaulu kwa daraja "A". Hata wanaofaulu kwa daraja "B" ni wachache.
Mchanganuo wa matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Upimaji Darasa la Saba mwaka 2021 katika Shule ya Msingi Lipumba. CHANZO: NECTA.
Kinachoshuhudiwa katika Shule ya Msingi Lipumba pia kinakinzana na miongozo ya kitaifa kielimu, ikiwamo Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 inayoitegemea Sekta ya Elimu, ambayo 'karakana' yake mojawapo ni shuleni Lipumba, iisaidie.
Dira hiyo inaipa jukumu Sekta ya Elimu na Mafunzo kunoa rasilimaliwatu kitaifa ili kuwa na watanzania mahiri walioelimika ili kuliletea taifa maendeleo endelevu na kuliweka kwenye uchumi shindani duniani.
Hali ya miundombinu shuleni Lipumba pia ni ishara ya kutofanyiwa kazi mapendekezo ya CAG aliyoyatoa kwa serikali miaka saba iliyopita.
Katika Ripoti ya Ukaguzi Maalumu wa Miundombinu na Samani kwenye Shule za Msingi Tanzania aliyoitoa Machi 2017, CAG (kipindi hicho Prof. Mussa Assad), anasema alibaini hali mbaya ya miundombinu na samani katika shule zinazomilikiwa na serikali.
Huku akidokeza kuwapo ongezeko la wanafunzi kwa wastani wa asilimia tano kila mwaka, CAG Assad alitoa mapendekezo ya maboresho, kwamba "serikali ichukue hatua za haraka kuboresha miundombinu iliyopo na kujenga mipya".
Ni uhalisia unaopata uthibitisho katika ripoti ya ukaguzi kwa mwaka 2020/21, ambamo CAG wa sasa, Charles Kichere, anasema ufuatiliaji wa utekelezaji mapendekezo ya Ripoti ya Ukaguzi Maalumu wa Mwaka 2017, umebaini "serikali inasuasua".
CAG Kichere anafafanua kuwa katika halmashauri 48 alizokagua, ikiwamo ya Mbinga iliko Shule ya Msingi Lipumba, amebaini uboreshaji miundombinu unasuasua.
"Kwa kuzingatia uchambuzi huu, ni wazi kwamba Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia hawakutekeleza kikamilifu mapendekezo yangu ya mwaka 2017.
"Hii inaweza kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia ufaulu duni wa wanafunzi wa shule za msingi nchini. Hali hii inadidimiza juhudi za serikali katika kuboresha elimu ya msingi na sekondari," CAG Kichere anabainisha.
Anapendekeza Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wafanye tathmini kuhusu dosari alizobaini ili kuboresha elimu ya msingi.
Hata hivyo, CAG Kichere ana angalizo kwamba, hilo litawezekana ikiwa Hazina itatoa fedha za kutosha na kuweka mikakati inayotekelezeka ili kukabiliana na dosari zilizobainika.
Kwa tathmini ya haraka, wanafunzi waliojiunga na elimu ya msingi mwaka 2017 baada ya ripoti hiyo ya CAG kutolewa, ndiyo wahitimu wa darasa la saba mwaka huu, ambao juzi walipangiwa shule za kujiunga kidato cha kwanza mwakani.
Katika kipindi hicho cha miaka saba, hali mbaya ya miundombinu shuleni Lipumba haijapata mageuzi stahiki. Hata kidogo kinachofanyika sasa shuleni ni juhudi za wanakijiji kukabili magumu yao kwa ujenzi wa vyoo na darasa. Serikali inaendelea na ujenzi wa darasa moja ndani ya miaka saba ya utekezaji hoja ya CAG.
Wakati Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Joseph Kashushura akitoa ufafanuzi kuwa hana bajeti ya kutosha kutatua matatizo hayo ya Lipumba na shule nyinginezo zilizomo katika himaya yake, taarifa rasmi za kiserikali zinaonesha kupotea mabilioni ya shilingi ambayo yangetumika kuboresha miundombinu shuleni.
Mtazamo huo wa fedha za umma kufanyiwa ubadhirifu, hata kusababisha pengo la ufanisi kwenye huduma za umma, unawasilishwa kupitia Uchambuzi wa Ripoti ya CAG kwa Mwaka 2022/23 uliofanywa na taasisi ya WAJIBU.
Kwa mujibu wa WAJIBU, chombo kinachosimamiwa na CAG mstaafu Ludovick Utouh, mwanazuoni wa uhasibu, imebainika miamala mbalimbali yenye viashiria vya rushwa, ubadhirifu na udanganyifu wa fedha za umma, inayofikia Sh. trilioni 11.857 ndani ya miaka minne (2019/20 - 2022/23).
Hapo panatolewa ufafanuzi namna Sekta ya Elimu inaathirika kwa tafsiri: "Kiasi hicho kama kingeelekezwa kutatua uhaba wa miundombinu shuleni, kingetosha kujenga vyumba vya madarasa mpya 592,850.
"Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), chumba kimoja cha darasa kinajengwa kwa Sh. milioni 20 kikiwa na samani zake zote."
Mwenendo wa viashiria vya rushwa, ubadhirifu na udanganyifu kuanzia mwaka 2019/20 hadi 2022/23. CHANZO: Ripoti ya Uwajibikaji ya taasisi ya WAJIBU. Uk. 4;
Kimsingi, uhaba wa miundombinu na samani shuleni Lipumba na kwingineko nchini, unakwaza utekelezaji Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22-2025/26).
Katika Sekta ya Elimu, mpango huo unaelekeza ifikapo mwaka 2026, mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule za msingi na sekondari yawe yameboreshwa kama vile ujenzi wa vyumba vya madarasa na ununuzi wa madawati.
Hali kadhalika, unagusa kuboreshwa uwiano wa vyoo na mazingira ya kazi kwa walimu katika ngazi zote na makazi yao kuwa karibu na maeneo ya kazi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED