MBIO za kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) zimezidi kunoga baada ya jana mwanachama mwingine kujitosa kuwania nafasi hiyo.
Mwanachama huyo kutoka tawi la Kunduchi Mtongani, Dar es Salaam ni Romanus Mapunda. Alifika katika ofisi za makao makuu ya chama hicho jana mchana kuchukua fomu.
Romanus anafanya idadi ya wanachama waliochukua fomu ya kuwania nafasi hiyo kuwa wawili baada ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Tundu Lissu kuchukua na kurejesha.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu, Romanus alitamba ataleta ushindani katika uchaguzi huo. Ana uhakika wa kushinda kwa sababu ana kundi kubwa la watu wanaomuunga mkono.
“Nimeamua rasmi kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya uenyekiti wa CHADEMA, nina sababu nyingi sana zilizonisukuma. Nimeona nina sifa ya kuwa mwenyekiti wa chama hiki na nina wadau wa kutosha na kuniunga mkono na ninaamini nitashinda, wadau wamenichangia fomu na kesho (leo), nitarudisha fomu," alisema.
Akichaguliwa kukalia kiti hicho, atafanya makubwa ikiwamo kuweka mikakati mizuri ya chama hicho kushika dola katika Uchaguzi Mkuu ujao.
"Ninachowaahidi wanachama wa CHADEMA, kwanza waniamini. Pili, mimi ni mtu wa kuamsha popo, wajenge imani na mimi twende pamoja, mwaka 2025 tunakwenda kushinda uchaguzi na tunachukua nchi mapema kabisa," alisema.
Aliongeza: "Sisi tunategemea kushinda serikali, lakini hatuwezi kukitoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani kwa kuhubiri, tunatakiwa tukakitoe madarakani kwa kupiga kura."
Mwenyekiti Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe hajaweka wazi kama atagombea au la, anatarajia kutoa uamuzi wake kesho atakapozungumza na wahariri wa vyombo vya habari.
Juzi akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Mikocheni, Dar es Salaam, Mbowe alisema maombi yao kumshawishi atetee tena nafasi yake ameyapokea, lakini atafanya uamuzi baada ya saa 48.
Mbali na nafasi ya uenyekiti wa chama, nafasi zingine zinazogombaniwa ni Makamu Mwenyekiti Bara na Makamu Mwenyekiti Zanzibar.
Nyingine ni Katibu Mkuu Baraza la Wazee (BAZECHA) Bara, Naibu Katibu Mkuu Bara, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar na Mweka Hazina.
Zingine ni wajumbe watano wa baraza kuu ambao wanne ni kutoka Tanzania Bara na mmoja ni kutoka Zanzibar pamoja na wajumbe 20. Kati yao, 15 ni kutoka Tanzania Bara na watano kutoka Zanzibar.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED