JK afichua yaliyomkuta Tendwa akitekeleza wajibu

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 11:30 AM Dec 20 2024
 Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete.
Picha:Mtandao
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete.

RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, amefichua masahibu aliyoyapata aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, alipokuwa akitekeleza wajibu wake.

Wakati Kikwete akiibua hayo, Wiziri Mkuu Kassim Majaliwa, amewataka Watanzania kuendelea kumwombea Tendwa na kusema alikuwa kiongozi wa mfano wa kuigwa.

Akizungumza jana wakati wa ibada ya kuaga mwili wa Tendwa, aliyefariki mapema wiki hii katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam, Kikwete alisema wakati akitekeleza majukumu yake, aliwahi kufungiwa ndani ya ofisi za chama cha CUF Zanzibar, alipokwenda kufanya uhakiki lakini alisimamia msimamo wake.

Kikwete alisema Tendwa alikuwa na mchango mkubwa katika kujenga demokrasia ya vyama vingi katika nchi na kwamba haiwezekani kuzungumzia ustawi wake bila kulitaja jina lake.

Alisema alipigiwa simu na mmoja wa mtoto wa Tendwa kumjuza kwamba baba yake anaumwa na muda wote alikuwa anamtaja.

“Nikasema ninashukuru nikamuuliza hali yake inaendeleaje? Akasema  hali yake ni ngumu yuko chumba cha uangalizi maalumu (ICU). Niliahidi  kwamba nitatafuta nafasi nikamwone lakini nikawa nina safari, niliporejea nikasema ngoja nikamwone lakini nikapata taarifa ameshafariki.

“Msiba huu si wa familia tu ni wa kwetu sote. Niwape  faraja familia ya mfiwa hamko peke yenu. Tendwa nimefanya naye kazi. Aliteuliwa  mwaka 2001 mimi niliingia madarakani mwaka 2005 mwishoni na alimaliza kipindi chake 2013 baadaye nikamteua Jaji Francis Mutungi. Ninachoweza  kusema alikuwa na sifa ya kusema ukweli,” alisema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Majaliwa alisema: “Nimekuja hapa kutoa salamu za pole za Rais Samia Suluhu Hassan na za kwangu.  Tendwa alikuwa mtumishi wa umma katika ofisi mbalimbal na alikuwa mtumishi mwaminifu.

“Amefanya kazi yake vizuri sana katika vyama vya siasa hasa katika kipindi ambacho vyama vilikuwa vinajijenga.”

Majaliwa alisisitiza taifa limepata pigo kubwa na kwamba jukumu lililopo kwa sasa ni kuungana na wanafamilia kuenzi mazuri aliyoyafanya katika utumishi wake.

MUTUNGI AMLILIA

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alisema Tendwa alikuwa mwalimu wake katika mambo mengi, ikizingatiwa kwamba alipokea kijiti cha uongozi kutoka kwake na yuko kwenye nafasi hiyo mpaka sasa.

Alisema Tendwa alijitolea kuhakikisha msingi wa demokrasi unajengwa ipasavyo na alikuwa mweledi katika kipindi chake. Pia alisema Tendwa  alihakikisha ofisi inakuwa kiunganishi kwa vyama vya siasa.

“Mchango wake uliimarisha mazingira ya kisiasa amani na mshikamano vilitawala katika uongozi wake. Hatuwezi  kuzungumzia mfumo wa vyama vingi bila kulitaja jina lake” alisema Mutungi

ACT WAZALENDO

Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu alisema wataendelea kumkumbuka Tendwa kama kiongozi aliyesimamia vyama kwa uadilifu mkubwa.

“Tutamkumbuka kama kiongozi mlezi aliyesiamamia vyama kwa uadilifu na weledi mkubwa, kiongozi aliyesimamaia demokrasia ndani ya vyama na nje. “Kumuenzi Tendwa ni sisi viongozi kuendelea kuyasimamia aliyoacha na kuvikuza vyama siasa na demokrasia ya kweli” alisema.

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ally Khatibu, alisema Tendwa alikuwa nguzo ya mazungumzo ya kitaifa na mshikamano wa kisiasa kwa kuwa aliongoza kwa hekima na kujenga mazingira ya siasa yenye heshima, usawa, na mshikamano baina ya vyama vya siasa.

“Katika nafasi yake kama Msajili wa Vyama vya Siasa, Tendwa alitoa mchango mkubwa katika kuimarisha misingi ya demokrasia ya vyama vingi. Alisimamia taratibu za vyama kwa haki na bila upendeleo, akijenga imani kati ya wadau wa siasa na wananchi,” alisema.

Viongozi Wengine walioshiriki kuaga mwili wa Tendwa ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderiananga, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dk. Jim Yonaz.

Kwa mujibu wa ratiba ya msiba huo iliyotolewa na familia juzi inaonesha Tendwa anazikwa leo katika makaburi ya Ununio kwa Kondo Dar es Salaam.