Ramadhan Brothers wapeleka tuzo Mlima Kilimanjaro

By Mary Mosha , Nipashe
Published at 12:54 PM Apr 30 2024
kundi la The Ramadhan Brothers.
PICHA: MAKTABA
kundi la The Ramadhan Brothers.

NYOTA wawili wa Tanzania wanaounda kundi la The Ramadhan Brothers, ambao walitwaa ushindi wa jumla katika shindano la kusaka vipaji la la America's Got Talent (AGT) Fantasy-Legue, wameanza safari ya siku sita kupanda Mlima Kilimanjaro, kuupeleka ushindi huo juu ya kilele cha Uhuru chenye urefu wa mita 5,895 kutoka usawa wa bahari.

Wanamichezo hao, Fadhil Ramadhan na Ibrahim Job, jana walianza kupanda mlima huo kupitia lango la Marangu.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu ambaye aliongoza viongozi wa serikali na watu mbalimbali kuwapokea nyota hao katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), alisema ujio wa kikundi hicho chenye vijana wawili wa kitanzania unaashiria vijana waweza kufanya vyema  ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

"Tumewapokea mkoani hapa kwa ajili ya kutembelea vivutio vilivyopo mkoani hapa na mikoa ya jirani, karibuni sana na mkawe chachu ya kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi kwa kupitia mtandao mbalimbali,” alisema Babu. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, vijana hao akiwamo Fadhili Ramadhan, alisema siri kubwa iliyowafikisha hapo ni kumcha Mungu, jitihada na mazoezi.

Alisema haikuwa ghafla wao kufika walipo na badala yake walianza kuonyesha kipaji chao ndani  ya nchi iliyowapelekea kuona fursa ya kufika huko na kunyakuwa ushindi.

"Licha ya kushinda ila  bado tutarudi kutetea ushindi wetu baina ya washindi waliopatikana, hivyo bado tunakazi ya kuendelea kufanya, ila tuwaase vijana kutokata tamaa, kuachana na kuiga mila na desturi mbaya kwenye mitandao ya kijamii na badala yake kuitumia kupata fursa na kujiletea kipato, mitandao ni mizuri sana na inaweza kuleta tija kwako, familia yako na taifa kwa ujumla," alisema Ibrahim Job.

Akizungumza baada ya kuwapokea, Mkurugenzi wa ZARA Adventures Beni, alisema vijana hao watakaa mkoani Kilimanjaro kwa siku 10, watapanda Mlima Kilimanjaro na kutembelea Hifadhi ya Serengeti.

Kikundi hicho cha vijana wa kitanzania kilijinyakulia kitita cha Dola za Marekani 250,000 baada ya kuwashinda wengine tisa waliofika fainali.