MAHAKAMA Kuu Masjala ya Wilaya, Arusha imeahirisha hadi Mei 6, mwaka huu shauri linalomkabili msanii wa muziki wa kizazi kipya (Bongo Fleva), Omary Mwanga, maarufu Marioo, na Meneja wake Sweetbert Mwinula, wanaodaiwa zaidi ya Sh. milioni 500 kwa kuvunja mkataba.
Shauri hilo liliahirishwa kwa sababu Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza shauri hilo hakuwapo mahakamani.
Mdai katika shauri hilo ni Kampuni ya Kismaty inayojihusisha na kuandaa matukio ya burudani mbalimbali nchini. Inawakilishwa na Wakili John Lairumbe. Upande wa mdai ulifika mahakamani, lakini wadaiwa hawakufika mahakamani.
Marioo na Meneja wake Sweetbert wakifunguliwa shauri, wakidaiwa jumla ya Sh. 550,000,000 kwa kuvunja mkataba wa kutumbuiza katika hafla ya Mr & Miss Vyuo Vikuu Kanda ya Kaskazini.
Inadaiwa kuwa Septemba 23, 2021, mdai aliingia mkataba na wadaiwa wa kutumbuiza siku ya mashindano hayo kwa gharama ya Sh. milioni 15.
Inadaiwa tukio lilitakiwa kufanyika Septemba 24, 2021 Arusha na Septemba 25, mwaka huo kulikuwa na hafla Blue Stone Lounge.
Inadaiwa kampuni hiyo, Septemba 17, mwaka huo iliwalipa wadaiwa Sh. milioni nane na wakati wakitia saini mkataba iliwalipa Sh. milioni 15.
Inadaiwa Septemba 25, 2021, hawakuonekana kwa ajili ya kutumbuiza Blue Stone kama walivyokubaliana katika mkataba.
Kutokana na kuvunja mkataba, mdai aliingia hasara ya Sh. milioni 500 na hasara nyingine ya Sh. milioni 50,000,000 ambayo ilipatikana kutokana na kukaribisha wadau mbalimbali wakiwamo wenye hoteli kubwa, fedha walizolipwa, alipoteza biashara na kukosa kipato.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED