JESHI la Polisi liliimarisha ulinzi Mlimani City, Dar es Salaam ulikofanyika Mkutano Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) huku magari ya jeshi hilo yakiwa yameegeshwa kwenye eneo hilo la kibiashara.
Wakati polisi wakiwa wametanda kwenye eneo hilo, wafuasi wa chama hicho walikuwa wamefurika nje na ndani ya jengo hilo wakiwa wameshika mabango ya wagombea wanaowania nafasi mbalimbali.
Wafuasi hao wa pande mbalimbali walisikika wakiimba nyimbo mbalimbali za kuwanadi wagombea wao huku wakiwa wameshika mabango yenye sura zao.
Baadhi ya wafuasi hao walisikika wakiimba: "Heche... Lissu... Heche... Lissu... Heche... Lissu..." wakiwa na maana wanamuunga mkono Lissu na Heche katika uchaguzi huo.
Ulinzi pia uliimarishwa kwenye milango ya kuingia ukumbini, hakuna aliyeruhusiwa kuingia pasi na kuwa na kadi maalum ya mwaliko, wahusika wakidai kuwa walifanya hivyo ili kudhibiti mamluki katika uchaguzi huo.
Pamoja na hayo, ubishani mkali ulizuka nje ya viunga vya ukumbi, pande mbili zikirushiana maneno na tambo -- upande mmoja ukitamba Lissu atashinda, na mwingine ukitamba Mbowe atashinda.
NJE YA UKUMBI
Nje ya ukumbi huo, baadhi ya wanachama waliokuwa wanawaunga mkono Lissu na Mbowe, walisema pamoja na kuwapo upinzani mkubwa kati ya viongozi hao, yeyote atakayeshinda wako tayari kumuunga mkono kwa maslahi ya chama.
Mmoja wa wanachama hao, Idrisa Mwakibete kutoka Mbeya, alisema anamuunga mkono Lissu kwa madai ni mpenda haki na ni jasiri anayeweza kukivusha chama kutoka kilipo.
"Ninatamani Lissu ashinde kwa sababu Mbowe hana jipya kwa sasa kwa miaka aliyoongoza inatosha kabisa, apumzike awaachie wengine majukumu," alidai.
Mwenyekiti wa CHADEMA Musoma Vijijini, Kasimu Mkoyo, alisema yeyote atayeshinda uchaguzi huo, atampokea kwa kuwa wote ni viongozi wanaowaamini.
Katibu wa Jimbo la Musoma Magharibi la CHADEMA, Musa Kamindawa, alisema chama chao kina hazina kubwa ya viongozi na yeyote atakayeshinda anaweza kufanya jambo kubwa kwa maslahi ya wanachama na nchi kwa jumla.
"Mimi kama mjumbe, ninaona kama ni funzo kwa taifa katika demokrasia baada ya uchaguzi, ninaiona CHADEMA ikiibuka kwa uimara zaidi.
"Haiwezi kugawanyika vipande, sioni kama hicho kitatokea kwa sababu hakuna aliyeonesha dalili kama akishinda atahama chama.
"Odero, Lissu na Mbowe wote ni waaminifu japo ushindi unaelemea kwa hao wawili, tunaamini tutaungana pamoja, kuwapo makundi ni kitu cha kawaida," alisema.
Mmoja wa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CHADEMA, Beatrice Ngongani, alisema alikuwa amejipanga kupiga kura, akiahidi kuchagua kiongozi mwenye hoja za kukivusha chama kutoka kilipo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED