Hofu yatanda kuibuka mpasuko CHADEMA

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 09:54 AM Jan 22 2025
Freeman Mbowe na Tundu Lissu.

WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wameingiwa na hofu ya kuwapo hatari ya chama hicho kupasuka au kuimarika zaidi baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa ndani wa kuwapata viongozi.

Walisema hayo jana Dar es Salaam kwa nyakati tofauti wakati wakijiandaa kuwachagua viongozi wa juu wa chama hicho wakiwamo Mwenyekiti na Makamu Wenyeviti Bara na Zanzibar.

Wanachama hao waliiambia Nipashe kuwa haijawahi kutokea tangu chama hicho kianze kufanya uchaguzi wa ndani wa viongozi wakuu kuwa na ushindani mkubwa kiwango hicho.

Wanaogombea nafasi ya uenyekiti ni Freeman Mbowe anayetetea nafasi hiyo, Tundu Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti hadi jana na Charles Odero.

Kwa nyakati tofauti, wajumbe hao walisema uchaguzi wa mwaka huu umekuwa na mvuto mkali kutokana na kugonganisha vigogo wawili ambao ni nguli na wanaokubalika katika kisiasa.

Baadhi ya wanachama wajumbe wa mkutano huo mkuu walisema hawajawahi kukutana na uchaguzi wenye upinzani ndani ya chama hicho kama ilivyokuwa awamu hiyo.

Mjumbe kutoka Manyara, Regula Mtei, alisema haijawahi kutokea kwenye uchaguzi uliopita kutokea na ushindani mkali kama ilivyotokea katika uchaguzi wa awamu hii.

"Na hii imetokea kwa sababu wamesimama manguli wawili. Uchaguzi huu umeleta mvuto ndani na nje ya CHADEMA kwa sababu ni watu wanaojua siasa, wanafanya siasa kama zinazofanyika duniani," alisema Regula.

Alisema uchaguzi wa mwaka huu hautabiriki kutokana na nguvu kubwa iliyopo kwa pande mbili za wagombea.

"Hatuwezi kutabiri kwa sababu uchaguzi una gharama zake, lakini tunachoamini ni kwamba lolote litakalotokea chama na msingi uliowekwa ndani ya chama utasaidia kukiimarisha tena," alisema.

Mjumbe kutoka mkoa wa Mbeya, Masaga Karoli, alisema: "Mimi nilishiriki uchaguzi wa mwaka 2019 ambao haukuteka hisia za watu lakini huu umeteka hisia nje na ndani ya chama kwa sababu umewakutanisha nguli wawili, wanye mtaji mkubwa wa kisiasa. 

 "Lakini nimesikiliza hotuba za wagombea. Nimeiona  nia ya dhati ya kutuunganisha baada ya uchaguzi isipokuwa wasiwasi wangu upo kwa hawa wapambe wanaounga mkono wagombea maana kuna baadhi wameingia na matokeo yao mfukoni kwamba lazima fulani ashinde. Sasa  hao ndio wenye shida kwa sababu ukiingia namna hiyo halafu ikawa ndivyo sivyo, inaweza kukuletea shida.”

Mjumbe kutoka Kisesa Mkoa wa Simiyu, Fabian Masunga, alisema ni jambo la busara sana kwa atakayeshinda na atakayeshindwa, hivyo  wakubaliane na matokeo na washikane mikono.

"Lissu tunampenda na Mbowe tunampenda na ndiyo wametufanya tufikie hapa leo ila uchaguzi wa leo ni 50/50 tuwe hapa leo na kama CHADEMA itafanikiwa kutoka salama hapa, itakwenda kuwa kubwa zaidi," alisema Masunga.

Mjumbe kutoka Siha, Filbert Mmari, alisema chama hicho kimefanya uchaguzi ambao umeweka historia kutokana na mvuto wake na aina ya watu wanaogombea.

"Hii miamba inayoshiriki uchaguzi imesababisha kuleta historia ambayo haijawahi kutokea ndani ya chama chetu. Hii  imesaidia pia kuonesha kwamba demokrasia ndiyo inatakiwa kuwa namna hii. Tunachoombea  ni kwamba chama kiendelee kubaki salama kwa sababu sisi wengine hatuna chama kingine cha kwenda," alisema Mmari.

Mjumbe kutoka Mjini Unguja, Abeid Haji Abeid, alisema uchaguzi uko vizuri isipokuwa anachokiona ni wapambe au ushabiki wa nje kuwa mkubwa na kusababisha taharuki.

Mjumbe kutoka Pemba, Habib Ali Khamis, alisema uchaguzi wa sasa umewafundisha jambo kubwa na kwamba kuanzia kundi la wajumbe wachache wa mkutano ambao ndio wanawaaminisha wengine wasio wapiga kura lakini anaamini chama hicho kitatoka salama.

Naye mjumbe kutoka Bunda, Samson Kandole, alisema huko alikotoka wanachama wamemtuma na kumpatia maelekezo mtu wa kumchagua na kwamba endapo matokeo hayatakuwa sawa na yule waliyemtaka, wako tayari kuacha chama na kuahirisha nafasi zote walizokuwa wamepanga kugombea kupeperusha chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani ikiwamo za ubunge na udiwani.

Kamuli Elias kutoka Bunda, alisema chama kina wakati mgumu kuhakikisha kinavuka salama baada ya uchaguzi.

Kabla ya kuanza kupiga kura, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John alitangaza kuwa Lissu kumteua Godbless Lema kuwa wakala wake.

Mnyika pia alitangaza kufanyika uhakiki wa wajumbe, huku kukiwa na madai ya kuwamo ukumbini watu wasiokuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu. Waliothibitika kutokuwa wajumbe, waliondolewa ukumbini.