Lissu atangaza msimamo kuhusu matokeo ya uchaguzi

By Restuta James , Nipashe
Published at 10:04 AM Jan 22 2025
Wakala wa Tundu Lissu Godbless Lema akifurahia baada ya Lissu kushinda katika uchaguzi huo.

KABLA ya uchaguzi wa viongozi wa kitaifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mgombea uenyekiti, Tundu Lissu alizima uvumi wa mitandaoni kwamba atakihama chama hicho asiposhinda.

Alisema yuko tayari kupokea matokeo yoyote na kwamba hata akishindwa atabakia ndani ya chama hicho.

Alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akitoa salamu zake mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanya uchaguzi wa viongozi wa kitaifa na wajumbe wa Kamati Kuu.

Lissu alisema pamoja na kutofautiana na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kwa misimamo lakini hawajawahi kugombana.

"Ndugu zangu na wajumbe wenzangu, huu ni mkutano wangu wa kwanza ndani ya chama ninaouhudhuria tangu mwaka 2014. Hii ni kwa sababu katika Mkutano Mkuu wa 2019, nilikuwa ninatibiwa Ubelgiji kufuatia tukio la jaribio la mauaji dhidi yangu Septemba 7, 2017," alisema.

Alikumbusha kuwa pamoja na kwamba alikuwa kitandani, aliomba kura ya kuwa Makamu Mwenyekiti Bara na wajumbe walimchagua kwa asilimia 98.8 ya kura 941 zilizopigwa siku hiyo.

Lissu alisema kuwa mwaka 2020 wajumbe hao walimpitisha kwa asilimia 100 ya kura na kumwidhinisha kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema huo ni ushahidi kwamba wajumbe walimchagua kutokana na imani yao kwenye uwezo wake.

"Niseme nini kwenu! Kwa watu ambao mmenipenda kiasi hiki, watu ambao mmenipa fadhila nyingi... vyovyote itakavyokuwa leo (jana), tutakuwa pamoja kujenga chama chetu," alisema Lissu huku akishangiliwa na wajumbe.

"Leo ninamaliza miaka yangu mitano, ninapenda kuamini nimewatumikia, nimekitumikia chama chetu na nimewatumikia wananchi wetu kwa namna ambayo tuna haki ya kujivunia," alisema.

Kuhusu uhusiano wake na Mbowe, Lissu alisema amekuwa naye bega kwa bega kwa miaka 20 na hajawahi kugombana naye.

Lissu alisema: "Tunaweza kuwa tumetofautiana kimsimamo, lakini hatujawahi kugombana".

Alisema anaamini kwamba uhusiano wake na Mbowe utaendelea kama zamani baada ya uchaguzi huo.

"Nitayasema hayo hayo kwa viongozi wenzangu wa chama. Tunaweza kuwa tumetofautiana kimsimamo, lakini hatujawahi kugombana. Ninaomba nitumie nafasi hii kuwashukuru nyote kwa miaka hii 20 ya utumishi wangu ndani ya chama chetu," alisema.

Lissu alisema kuwa uamuzi wowote utakaofanywa na wajumbe wa chama hicho ni sehemu ya ujenzi wa chama, naye ni muumini wa ujenzi wa chama hicho.

WAJUMBE WAMSHANGILIA

Alipoitwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika kutoa salamu zake, wajumbe walilipuka kwa shangwe wakiimba "Lissu... Lissu... Lissu..."

Lissu alichuana na Mbowe na Charles Odero kwenye nafasi ya uenyekiti. Nafasi nyingine iliyokuwa na mchuano mkali katika uchaguzi huo ni ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, washindani wakiwa ni John Heche anayemuunga mkono Lissu na Ezekia Wenje aliye upande wa Mbowe.

Kwa upande wa Tanzania Zanzibar, wanaogombea Umakamu Mwenyekiti wa Chama, ni Hafidh Ali Saleh, Suleiman Makame Issa, Said Issa Mohammed na Said Mzee Said.