...Uteuzi CCM wawaibua wadau

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:05 AM Jan 21 2025
Uteuzi CCM wawaibua wadau.
Picha: CCM
Uteuzi CCM wawaibua wadau.

WADAU wa siasa wamesema uamuzi wa kupata wagombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mapema ni turufu kwa chama, huku wakisifu uteuzi wa Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza.

Mchambuzi wa masuala ya siasa na uchumi nchini, Dk. Albanie Marcossy, alisema uamuzi wa kuwapata wagombea kwa kushtukiza na mapema ni ishara uchaguzi ujao hautakuwa mwepesi.

Askofu wa Kanisa la Baptist Tanzania Kanda ya Kati, Antony Mlyashimba, alisema Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM umefanya jambo jema kwa mujibu wa kanuni za chama hicho, majina ya wagombea yamefahamika mapema. Itawasaidia wanachi kuwafahamu vizuri ili kuwachagua kwenye Uchaguzi Mkuu.

"Jambo lililofanywa na chama hiki ni zuri, kama inawezekana ipo haja ya kubadilishwa kwa sheria, ili michakato hii ianze mapema kwa vyama vyote kutambulisha wagombea wao ili wafahamike na wapigakura wao. Mgombea wa nafasi ya urais si vizuri kuwa wa kushtukiza, lazima tumjue mapema.

"Maana hata wenyewe CCM jana (juzi) kwenye mkutano wa kupitisha majina hayo kulikuwa na sintofahamu, hivyo ipo haja kama kuna uwezekano kufanyike marekebisho, ili kusiwe na ukakasi kama uliotokea jana maana hata Rais mstaafu Jakaya Kikwete hakuwa na majibu ya moja kwa moja," alisema.

Hassani Mbangile, mkazi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, alisema demokrasia ndani ya CCM inapaswa kuzingatia taratibu za ndani za chama hicho.

Alisema chama hicho kilipaswa kutoa nafasi kwa wagombea wengine kugombea nafasi ya urais badala ya kupitisha jina moja la mgombea wa urais, jambo ambalo anaona ni kuminya haki za wanachama wengine ambao wanataka majukumu hayo.

Mkuu wa Kitivo cha Ushirika na Maendeleo ya Jamii ya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Dk. Cyril Komba, akizungumzia uteuzi huo na sura yake kisiasa nchini alisema:

“Hii inaonesha jinsi gani CCM iko makini. Kwa uteuzi wa Balozi Dk. Nchimbi, Rais Samia Suluhu Hassan au CCM imefanya jambo la maana sana. Nchimbi amekulia kwenye chama tangu akiwa kijana.

"Hakuna asiyefahamu umahiri wake katika kukisaidia chama kishinde uchaguzi, amekuwa ni nguzo kuu katika ushindi wa CCM tangu akiwa kijana Umoja wa Vijana (UVCCM), akawa waziri, balozi na sasa Katibu Mkuu wa Chama. Kwa hiyo nafikiri chama kimelamba dume."

Mkazi wa jijini Dodoma, Bashiru Kajuna, pia alipongeza mkutano mkuu kwa kupitisha jina Balozi Nchimbi, kuwa mgombea mwenza kwenye Uchaguzi Mkuu 2025.

Mwanazuoni na mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka jijini Mwanza, Pius Lufutu alisema hatua hiyo ya juzi ya CCM ni mkakati katika kuufikia mchakato wa uchaguzi.

Alisema kuwa kwa mujibu wa chama hicho, mabadiliko yoyote ya kikatiba yanaweza kufanyika muda wowote kutokana na makubaliano ya kamati kuu za chama hicho.

"Tunaweza kujiuliza kwanini wamefanya mapema hivi badala ya utaratibu wa kawaidi wa mwezi Mei, majibu ni kuwa kwa upande wa CCM wenyewe wamefuata matakwa ya kikatiba kuwashirikisha wajumbe wote wa kamati tendaji ya chama hicho ambao wameridhia mabadiliko madogo kwa manufaa  ya chama," alisema.

*Imeandikwa na Godfrey Mushi (ARUSHA), Paul Mabeja (DODOMA), Vitus Audax (MWANZA) na Baraka Jamali (MTWARA).