Kishapu wapitisha makadirio bajeti bil 41.4/- mwaka 2025/26

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 07:35 PM Jan 21 2025
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu,Francis Manyanda, akizungumza kwenye baraza hilo la bajeti
Picha: Marco Maduhu
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu,Francis Manyanda, akizungumza kwenye baraza hilo la bajeti

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, wamepitisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Sh. bilioni 41.4, huku wakipongeza taarifa ya bajeti hiyo kuwa na uwazi na wameweza kuichangia vizuri.

Wamepitisha bajeti hiyo leo, Januari 21, 2025 kwenye Kikao cha Baraza cha Bajeti katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.

Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Emmanuel Johnson, akisoma taarifa hiyo ya makadirio ya mapato na matumizi katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, amesema wameomba kuidhinishiwa kukusanya kiasi cha fedha sh. bilioni 41.4 kutoka mapato ya ndani, serikali kuu na wadau wa maendeleo.

"Mheshimiwa Mwenyekiti katika mwaka wa fedha 2025/2026, halmashauri inaomba kuidhinishiwa kukusanya kiasi cha fedha Sh. bilioni 41.4," amesema Johnson.

Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, wapitisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti
Amewapongeza pia madiwani kwa kujadili taarifa hiyo vizuri na kutanguliza maslahi ya wananchi, na kwamba ushauri,maelekezo na mapendekezo yote ambayo wameyatoa atayafanyia kazi.

Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Andrew Kifua, akitoa salamu za viongozi kwenye baraza hilo, amewapongeza madiwani wa kujadili vyema na kuipitisha bajeti hiyo.

Amepongeza pia hoja za kuibua vyanzo vipya vya mapato na kuwasihi watendaji wa halmashauri wakasimamie vizuri vyanzo hivyo, ili halmashauri ipate mapato.

Aidha, katika Baraza hilo la Madiwani walipitisha pia mpango wa mapendekezo ya bajeti ya matengenezo ya barabara (TARURA) katika mwaka huo wa fedha 2025/2026 kiasi cha Sh. bilioni 2.3.