Malasusa ataja kiini ndoa nyingi kuvunjika

By Christina Haule , Nipashe
Published at 09:46 AM Jan 21 2025
MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa.
Picha:Mtandao
MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa.

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa ameitaka jamii kusimamia maadili ya malezi na ulinzi kwa mtoto ili kumwepusha na ndoa za utotoni zinazochangia talaka nyingi kwa wanandoa nchini.

Askofu Dk. Malasusa alisema hayo jana jijini Mwanza wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini yaliyoandaliwa na KKKT kupitia Upendo Media chini ya mradi wa Hapana Marefu Yasiyokuwa na Mwisho.

Alisema ndoa za utotoni zinaondoa upendo kwa binadamu na ndio maana kuna tatizo kubwa la talaka nchini na hiyo ni kuonesha kuwa mmoja wa wanandoa hakuwa na uamuzi wa kuingia katika ndoa.

"Watoto wengi wanasukumwa katika ndoa huku wakiwa hawana uhuru wa kuingia huko na ndio maana kunakuwa na talaka nyingi kwa wanandoa kwa sasa," alisema Askofu Dk. Malasusa.

Alisema ana imani kuwa Tanzania imefaulu kwenye mambo mengi na hata hili wanahabari wakilichukulia kwa undani litakomeshwa.

Alisema wapo baadhi ya wazazi wanaokatisha ndoto za watoto wao kwa kuwaachisha masomo na wengine kuwalazimisha kufanya vibaya kwenye masomo ili waozeshwe, hivyo kuitaka jamii kusimamia na kuisaidia serikali kudhibiti kitendo hivyo.

Kiongozi huyo wa kiroho alisema wazazi wamekuwa wanaamua kujipatia umiliki wa mtoto, hasa pale wanapoona anapewa ubini wake, hivyo kuamua kumtumia watakavyo isivyo sahihi.

"Wengine wanaamua kumwuza kwa mahari kabla ya umri. Tuondoe fikra za watoto kuwa bidhaa, hawapo kwa ajili ya kuuzwa, tusimame pamoja kukemea vitendo hivi," alisema Dk. Malasusa.

Alisema watoto wanatakiwa kufunzwa juu ya haki zao wanazopaswa kuzisimamia na kujitetea kwa kujua kuwa wao wana maisha zaidi kuliko kukimbilia katika ndoa.

Mkurugenzi wa Upendo Media, Neng’ida Johannes alisema tatizo la ndoa za utotoni ni kubwa katika mikoa ya Dodoma, Shinyanga, Tabora, Mara na Lindi.

Aliwahimiza waandishi wa habari kuendelea kusemea maeneo yaliyoathirika ili kusaidia watanzania kuacha tabia za kuoza watoto wadogo.

Msimamizi Mkuu wa Program ya Maisha Endelevu na Uwezeshaji kutoka KKKT, Patricia Mwaikenda, alisema ni wakati sasa jamii kutamBua namba ya serikali 116 ili kutoa taarifa wanapobaini ukatili wa aina yoyote.

Mwaikenda alisema mradi huo unatekelezwa katika mikoa minne, ikiwamo ya Zanzibar na kupata wakufunzi 30 ukiwa na mitaala inayosimamia na vyuo vikuu vinne nchini sambamba na mafunzo kwa walimu 24 wa shule za awali mkoani Morogoro.

Alisema tangu mradi uanze mwaka 2023, mpaka sasa kanisa tayari limeshaokoa watoto watatu waliokuwa wanaozeshwa katika umri mdogo ambao hadi sasa wana mafanikio kielimu.