WAZIRI wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa amemtaka Mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa kipande cha tano cha reli ya kisasa (SGR) cha Mwanza-Isaka kuhakikisha anafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika vipande vilivyokamilika ili yasijirudie katika kipande hicho.
Prof. Mbarawa alitoa maelekezo hayo juzi alipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ( SGR ) kipande cha tano kutoka Mwanza-Isaka chenye urefu wa km 341 pamoja na stesheni kubwa ya Malampaka inayotarajiwa kutumiwa na mikoa ya Simiyu na Mara.
Alisema miongoni mwa changamoto zilizojitokeza katika maeneo ya Dar es Salaam, Morogoro pamoja na Dodoma ambako tayari uendeshaji wa mradi huo umeanza ni pamoja na ufinyu wa maegesho.
“Kwa Dar es Salaam mpaka Dodoma tulikuwa na changamoto ya maegesho awali tulifanya kwa makadirio ya watu kufika kwa awamu lakini imekuwa tofauti ilivyofunguliwa watu walikuja kwa wingi hivyo kwenye mikoa hii tuhakikishe tunajipanga vizuri hata kama ikitokea idadi ya watu ikaongezeka yawepo na maegesho ya vyombo vya moto ya kutosha nina imani hatujachelewa," alisema Prof.Mbarawa.
Kuhusu hatua za mradi huo Prof.Mbarawa alisema kwa jumla umefikia asilimia 63.04 na kuwa kazi iliyosalia ya asilimia zaidi ya 30 inayojumuisha uwekaji wa nguzo na kutandika reli aliyoitaja kuweza kufanyika wakati wowote hata wakati wa mvua.
Kadhalika alisema ujenzi wa tuta umefikia asilimia 89 huku upande wa muundo unaojumuisha madaraja pamoja na makaravati ukifikia zaidi ya asilimia 74 na kumpongeza mkandarasi kwa kazi anayoendelea nayo.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Masanja Kadogosa alisema ujenzi huo ulisitishwa kwa muda kutokana na mvua iliyokuwa ikinyesha na kuwa wanatarajia kuanzia mwezi wa nne kuanza kujenga kwa kasi zaidi.
Alisema kwa sasa wanaendelea na ujenzi wa stesheni kubwa za Shinyanga, Malampaka, Isaka pamoja na Mwanza na kuwa katika kipindi cha Mwenzi Novemba na Januari walipokea dola milioni 37 sawa na zaidi ya Sh.bilioni 95.6 zitakazosaidia kuendeleza kazi hiyo.
Meneja mradi huo Mhandisi Moga Kulwa alisema stesheni ya Malampaka itakuwa na uwezo wa kuhudumia watu 502 kwa wakati mmoja.
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Kenan Kihongosi alisema mradi huo utakuwa na tija katika kukuza uchumi wa nchi na utasaidia wananchi kupata unafuu katika kusafiri na kusafirisha mizigo pamoja na bidhaa mbalimbali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED