Wananchi wa kata ya Ukalawa Jimbo la Lupembe Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, wamekabidhiwa kituo cha afya kilichojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF na nguvu ya wananchi chenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 157.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa kituo hicho cha afya, mmoja wa wananchi hao akiwemo Pius Daniel amesema kuanza kutoa huduma katika kituo hicho kutasaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Mbunge wa Jimbo la Lupembe, Edwin Swalle amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kukamilisha kituo hicho na kwamba amewaokoa wananchi hao ambao walikuwa wanatembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amewapongeza wananchi wa kata hiyo kwa kujitolea nguvu zao kujenga kituo cha Afya huku akiwataka watoa huduma za afya kuwa na lugha nzuri kwa wagonjwa wanaofika kupata huduma katika kituo hicho.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Njombe Deo Sanga alisema ujenzi wa kituo hicho cha afya ni utekelezaji wa Ilani ya chama hicho na kueleza kuwa wataendelea kutatua changamoto za wananchi pindi zinapobainika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED