Hamas yawaachia huru mateka sita wa Israel

By Enock Charles , Nipashe
Published at 07:47 PM Feb 22 2025
Wananchi wa Israel wakifurahi wakati wakiangalia katika televisheni tukio la kuachiliwa kwa wapendwa wao
PICHA:MTANDAO
Wananchi wa Israel wakifurahi wakati wakiangalia katika televisheni tukio la kuachiliwa kwa wapendwa wao

Kundi la wanamgambo wa Kipalestina la Hamas limewaachia huru leo mateka sita wa Israel na kuwakabidhi kwa maofisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu huku Israel ikitarajiwa kuwaachia mamia ya wafungwa wa Kipalestina.

Mapema leo, Hamas iliwaachia huru kutoka Rafah mateka wawili wa Israel waliofahamika kama Tal Shoham na Averu Mengistuna. Mateka wengine wanne, Omer Shem-Tov, Eliya Cohen, Omer Wenkert, na Hisham al-Sayed, waliachiliwa baadaye huko Nuseirat katikati mwa Gaza.

Mateka wa sita aliyeachiwa mwishoni alifahamika kwa jina la Hisham al-Sayed (37) pia baadaye alikabidhiwa kwa Shirika la Msalaba Mwekundu. Hisham alikuwa akishikiliwa mateka na Hamas kwa zaidi ya miaka 10. Israel itatakiwa pia kuwaachilia mamia ya wafungwa wa Kipalestina wanaokadiriwa kufikia idadi ya 600.

Mabadilishano hayo ya mateka na wafungwa ni sehemu ya makubaliano ya usitishwaji mapigano huko Gaza. Hamas imesema Jumamosi kuwa iko tayari kutekeleza awamu ya pili ya mpango wa makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza, awamu ambayo itatakiwa kuendeleza hatua za kubadilishana mateka na wafungwa na kusitisha kabisa vita huko Gaza huku vikosi vya Israel vikijiondoa kabisa katika Ukanda huo.


CHANZO:MTANDAO