Wanaotaka urais CCM waonywa

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 08:36 PM Jan 21 2025

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Fadhili Maganya.
Picha: Paul Mabeja
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Fadhili Maganya.

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Fadhili Maganya amesema baada ya Mkutano Mkuu wa chama hicho, kupitisha majina ya wagombea urais, kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu zoezi hilo ndiyo limefungwa rasmi.

Amesema, kutokana na hali hiyo kwa mwanachama yeyote ambaye anaona hawezi kuishi bila urais basi anapaswa kwenda kuutafuta sehemu nyingine na siyo ndani ya CCM.
 
Maganya, amesema hayo leo jijini Dodoma, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maamuzi ya mkutano mkuu wa CCM, kuwapitisha Rais Samia Suluhu Hassan na Dk. Hussein Ali Mwinyi kuwa wagombea wa nafasi ya urais kwa Tanzania bara na Zanzibar.
 
“Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi Taifa inaunga mkono maamuzi ya mkutano mkuu ulifanyika jijini hapa mwishoni mwa wiki iliyopita, na kwa maamuzi hayo nitoe rai kwa wanachama wote wa CCM nchini kuwaunga mkono wagombea hawa na kuwatafutia kura za kutosha.
 
“Lakini kama kuna mwanachama ambaye yeye anaona kuwa hawezi kuishi bila urais basi nafasi hiyo ndani ya CCM haipo tena, labda akatafute urais kwenye taasisi zingine au kwenye vyama vya michezo huku pia zipo nafasi za uarais unaoanza na R ndogo”amesema Maganya