MAWAKALA wa Usalama wa Marekani jana walivamia jumba la rapa, Sean "Diddy" Combs au Puff Daddy lililoko Holmby Hills kwa ajili ya uchunguzi, huku yeye mwenyewe akitokomea kusikojulikana.
Sababu hasa ya uvamizi huo bado haijawekwa wazi, lakini P Diddy hivi karibuni amehusishwa na madai ya unyanyasaji wa kijinsia na biashara ya ngono.
Mawakala hao walivamia jumba hilo katika mtaa wa 200 wa S. Mapleton Drive huko Holmby Hills, eneo la matajiri la Los Angeles linalojulikana kama mitaa ya watu mashuhuri na jumba la Playboy.
Jumba hilo linahusishwa na Kampuni ya Utengenezaji wa Filamu za Bad Boy ya Combs.
Mawakala hao walionekana wakiwashikilia wanaume wawili ambao baadaye walitambuliwa kuwa ni watoto wa Diddy, na kwamba vijana hao walizuiliwa nje huku upekuzi ukiendelea ndani ya jumba hilo.
"Mapema leo (jana), uchunguzi wa Usalama wa nchi (HSI) New York, ulichukua hatua za kutekeleza sheria kama sehemu ya uchunguzi unaoendelea, kwa usaidizi kutoka kwa HSI Los Angeles, HSI Miami, na washirika wetu wa kutekeleza sheria katika eneo husika.
“Tutatoa taarifa zaidi kadri zitakavyopatikana," ilisema taarifa ya Idara hiyo ya Usalama wa nchi katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari.
Idara ya kipolisi ya Sheriff ya Los Angeles pia ilikuwapo katika kusaidia zoezi hilo.
Wanawake ambao wametoa shutuma hadharani dhidi ya Diddy wameonesha kufurahishwa na uvamizi huo wa nyumba za P Diddy.
Wakili Douglas Wigdor, anayemwakilisha Cassie Ventura na mlalamikaji ambaye jina lake lilijulikana kama Jane Doe, alitoa taarifa hii:
"Siku zote tutaunga mkono utekelezaji wa sheria unapotaka kuwafungulia mashtaka wale ambao wamekiuka sheria. Tunatumaini huu ni mwanzo wa mchakato ambao utamshikilia P Diddy kuwajibika kwa mwenendo wake potovu."
Majumba mawili yalifanyiwa uchunguzi huko Los Angeles na Miami kama sehemu ya uchunguzi.
Hata hivyo, wawakilishi wa rapa huyo hawakuwa tayari kuzungumzia zoezi hilo.
Pia, P Diddy mwenyewe imedaiwa kwamba aliondoka mapema kwa ndege binafsi kuelekea kusikojulikana.
Mwaka jana, mwimbaji wa R&B, Cassie, ambaye jina lake kamili ni Casandra Ventura, aliwasilisha kesi katika mahakama ya shirikisho ya New York dhidi ya Combs, ambaye walikuwa wamechumbiana kati ya 2005 na 2018.
Wanawake wengine wawili wakajitokeza na kesi zao, wakimtuhumu kwa unyanyasaji wa kijinsia.
Mwanamume mmoja pia amejitokeza akimtuhumu Combs kwa kumfanyisha kazi za kingono bila ridhaa yake.
P Diddy ndiye mwanzilishi wa Lebo ya Bad Boy Records na ni mshindi wa tuzo ya Grammy mara tatu ambaye amefanya kazi na wasanii wa kiwango cha daraja la juu kama Usher na Mary J Blige.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED