Mwinyi asema kauli zake si porojo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:07 AM Dec 22 2024
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi
Picha: Mtandao
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema mambo yote anayoyatamka hadharani kuhusu utekelezaji wa miradi mikubwa zaidi ya maendeleo, si porojo za kisiasa bali ni dhamira yake ya kweli ya kufikia azma hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Idara ya Mawasiliano Ikulu, Zanzibar, ilisema Rais Mwinyi alitoa kauli hiyo alipofungua maonesho ya kwanza ya ghorofa Malindi Zanzibar, Shehia ya Mchangani, wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni shamrashamra za miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Dk. Mwinyi alisema  kufanya hivyo ni kuonesha uongozi unaoacha alama na uzalendo pamoja na kuwahakikishia wananchi kwa kaulimbiu inayosema “Yajayo ni Makubwa Zaidi.”

Aliitaja miradi mingine mikubwa ya kimkakati inayotarajiwa kutekelezwa miaka ijayo chini ya uongozi wake kuwa ni pamoja na mradi wa teksi za baharini ambapo ujenzi wa bandari za teksi  hizo umeanza Maruhudi. 

Alisema teksi hizo zitapakia na kushusha abiria watakaotumia usafiri wa maji kuelekea maeneo ya mkoa wa Kaskazini Unguja badala ya usafiri wa nchi kavu wa daladala na usafiri mwingine.

 Miradi mingine, kwa mujibu wa Dk. Mwinyi, ni wa treni zitakazotumia barabara za lami kutoka Malindi mjini hadi Bububu, ujenzi wa barabara nne za juu zenye mapishano.

Dk. Mwinyi pia aliwatoa hofu wananchi wa Mji Mkongwe kwamba serikali inatekeleza miradi yake huku ikiwa na dhamira njema ya kuuendeleza urithi wa kimataifa kwa lengo la kuulinda mji huo na si kuuharibu.

Alisema uzinduzi wa maegesho ya magari Malindi una nia ya kupunguza msongamano wa magari makubwa na madogo yanayoingia na kutoka Mji Mkongwe. 

Dk. Mwinyi pia alibainisha kuwa mbali na maegesho hayo, nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kujenga kituo cha kisasa cha mabasi ya abiria pembezoni mwa maegesho ya gari Malindi, sambamba na ujenzi wa kituo kikubwa cha magari ya abiria na kiwanja cha michezo kwa vijana.

Alisema kupitia mradi wa “Big Z”, serikali pia inakusudia kujenga mradi wa barabara ya kisasa kutoka Malindi hadi hospitali ya Mnazi Mmoja ikiwa ni hatua ya kuupandisha hadhi Mji Mkongwe pamoja na kuwa na mradi wa kuweka nyaya zote za umeme, maji na mawasiliano chini ya ardhi ili kuimarisha usafi wa mji huo kwa kuikarabati upya kwa kuiboreshea haiba njema “Jamhuri Garden” ili iwe na mwonekano wa kisasa.

Aidha, Rais Mwinyi ameupongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kwa kutoa mafao kwa wananchi kwa wakati na kwa kiwango kizuri, kuwekeza kwenye miradi yenye tija na kufanikiwa kutoa mchango kwa maendeleo ya nchi kwa kujenga miradi mikubwa. Akitolea  mfano mataifa mengine duniani, alisema mifuko ya hifadhi ya jamii ndiyo inayojenga nchi, hivyo aliitaka ZSSF kuendeleza utaratibu huo.

Dk. Mwinyi pia aliwasisitiza wanachi kuendelea kuidumisha amani ya nchi, umoja na mshikamano ili nchi iendelee kupiga hatua kubwa za maendeleo.

Amempongeza mkandarasi Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) na Mshauri Elekezi kwa CCEC kwa kufanikisha ujenzi wa maegesho ya magari Malindi kwa viwango cha hali ya juu na kuzingatia wakati.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mita na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed, ambaye pia amemwakilisha Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Saada Mkuya Salum, alisema maendeleo anayoyafanya Rais Dk. Mwinyi, yamewafilisi watu wasioitakia mema Zanzibar.

Pia alisema wananchi watamkumbuka kwa kuacha alama ya uongozi wake na kuonesha uzalendo alionao kwa nchi.

Kuhusu gharama za ujenzi wa maegesho hayo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Dk. Juma Malik Akili, alisema Sh. bilioni 6.8 zilitumika na kuwasisitiza wananchi kuendelea kuwasilisha michango yao ZSSF ili miradi mikubwa zaidi ya maendeleo iendelee kutekelezwa na mfuko huo.

Katibu Mkuu alisema maegesho hayo yana uwezo wa kuchukua magari 200 hadi 220 kwa wakati mmoja.