Madiwani Shinyanga waidhinisha bajeti ya bilioni 44.9 kwa 2025/26

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 04:05 PM Jan 31 2025

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngassa Mboje akiongoza kikao cha Baraza la Madiwani cha kupitisha Rasmi ya Bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026 sh.bilioni 44.9.
Picha: Marco Maduhu
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngassa Mboje akiongoza kikao cha Baraza la Madiwani cha kupitisha Rasmi ya Bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026 sh.bilioni 44.9.

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wamepitisha Rasimu ya Mpango wa Bajeti ya Shilingi bilioni 44.9 kwa mwaka wa fedha 2025/2026 katika Kikao Maalumu cha Baraza la Bajeti kilichofanyika Januari 30, 2025.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ngassa Mboje, alisema bajeti hiyo imejikita katika kuboresha maisha ya wananchi na kuwa dira ya maendeleo ya halmashauri. "Nawauliza Madiwani, Rasimu hii ya Mpango wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 ya shilingi bilioni 44.9 katika Halmashauri yetu ya Wilaya ya Shinyanga, je mmeipitisha?" aliuliza Mboje, na madiwani wote wakaidhinisha kwa kauli moja.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Ibrahimu Makana, aliwapongeza madiwani kwa kujadili na kupitisha bajeti hiyo kwa umakini. Alielekeza menejimenti ya halmashauri kuhakikisha mapendekezo yaliyotolewa na madiwani yanaingizwa kwenye mfumo rasmi na kutekelezwa ipasavyo.

Aidha, aliagiza bajeti hiyo izingatie malipo ya watumishi wa afya na walimu wanaofanya kazi kwa mkataba wa muda, ili kuhakikisha haki zao zinalipwa.

Mbali na bajeti kuu, madiwani walipitisha bajeti za taasisi mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwemo:
SHUWASA – Shilingi milioni 825 kwa utekelezaji wa miradi ya maji.
TARURA – Shilingi bilioni 2.4 kwa matengenezo ya miundombinu ya barabara.
TANROADS – Shilingi milioni 773 kwa ujenzi wa barabara ya Old Shinyanga–Salawe (km 65) na shilingi milioni 140 kwa barabara ya Didia–Ntobo (km 8.4).