Mawaziri wa Ulinzi pamoja na Wakuu wa Majeshi wa nchi zinazochangia wanajeshi katika operesheni za kivita ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wameagizwa kwenda mstari wa mbele vitani ili kuhakikisha usalama wa wanajeshi wa Kikosi cha SADC nchini DRC (SAMIDRC) na kuwezesha urejeshaji wa miili ya wanajeshi waliopoteza maisha pamoja na kuwahudumia majeruhi.
Agizo hilo ni miongoni mwa maamuzi yaliyotolewa kwa kauli moja katika Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika tarehe 31 Januari 2025 kujadili hali ya usalama nchini DRC.
Mkutano huo uliofanyika mjini Harare, Zimbabwe, uliendeshwa na Mwenyekiti wa SADC ambaye pia ni Rais wa Zimbabwe, Dk. Emmerson Mnangagwa. Viongozi wa mataifa 13 wanachama wa SADC walihudhuria, wakiwemo kutoka Zimbabwe, Botswana, DRC, Madagascar, Msumbiji, Afrika Kusini, Tanzania, Zambia, Lesotho, Eswatini, Angola, Malawi na Namibia.
Hali ya Usalama Mashariki mwa DRC
Mkutano huo ulipokea taarifa za hivi karibuni kuhusu hali ya usalama Mashariki mwa DRC, ukieleza wasiwasi mkubwa juu ya mashambulizi yanayoendelea kufanywa na kundi la waasi la M23 kwa kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF). Mashambulizi haya yamewalenga wanajeshi wa serikali ya DRC, kikosi cha SAMIDRC, pamoja na raia wa Kivu Kaskazini.
Viongozi wa SADC walitoa salamu za pole kwa DRC, Malawi, Afrika Kusini na Tanzania kwa wanajeshi wao waliopoteza maisha katika mashambulizi ya hivi karibuni huko Sake, Mashariki mwa DRC, huku wakitamani majeruhi wapone haraka.
Hatua za Kurejesha Utulivu
Viongozi hao walieleza wasiwasi wao kwamba mashambulizi haya yameendelea kuzorotesha hali ya usalama na kusababisha mgogoro wa kibinadamu nchini DRC. Walisisitiza kurejeshwa mara moja kwa huduma muhimu kama maji, umeme, mawasiliano, pamoja na njia za usambazaji wa chakula na bidhaa nyingine muhimu.
Aidha, walilaani vikali mashambulizi yanayofanywa na waasi wa M23 dhidi ya wanajeshi wa SAMIDRC, wakisema kuwa vitendo hivyo vinakiuka makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Mchakato wa Luanda mnamo Julai 30, 2024. Mashambulizi hayo yanahatarisha juhudi za kurejesha amani na usalama katika DRC na ukanda mzima wa SADC.
Mkutano huo ulikumbusha uamuzi wa Mei 2023 wa kupeleka kikosi cha ulinzi wa amani nchini DRC kusaidia juhudi za kurejesha amani na kulinda mipaka ya nchi hiyo. Hata hivyo, mkutano ulibainisha kuwa malengo haya bado hayajafikiwa kikamilifu.
Juhudi za Kidiplomasia na Ushirikiano wa Kikanda
Viongozi wa SADC walisema wataendelea kuunga mkono juhudi za kidiplomasia kutafuta suluhisho la kudumu kwa mgogoro wa DRC kupitia Mchakato wa Luanda unaoongozwa na Rais wa Angola, João Manuel Gonçalves Lourenço, pamoja na Mchakato wa Nairobi, uliokuwa chini ya Rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta.
Pia, mkutano huo uliitisha kikao cha dharura cha wakuu wa nchi wanachama wa SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kujadili hatua za kuchukua kuhusu usalama wa DRC, kufuatia maazimio ya Mkutano wa 24 wa Wakuu wa Nchi wa EAC uliofanyika tarehe 29 Januari 2025.
Kwa upande mwingine, SADC iliagiza Troika ya Siasa, Ulinzi na Usalama kushirikiana na pande zote zinazohusika katika mgogoro wa DRC ili kuratibu usitishaji mapigano, kulinda maisha ya raia, na kuhakikisha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kwa jamii zilizoathirika.
Ushirikiano wa Kisiasa na Kijeshi
Viongozi wa SADC waliwataka viongozi wa kisiasa na kidiplomasia wanaohusika na mgogoro huo kushiriki kikamilifu katika mazungumzo ya amani, ikiwa ni pamoja na kushirikiana na MONUSCO na wadau wengine wa kimataifa ili kurejesha utulivu Mashariki mwa DRC.
Aidha, Wakuu wa Nchi walisisitiza mshikamano wao na kujitoa kwa dhati kuendelea kuiunga mkono DRC katika kulinda uhuru wake, mamlaka yake, na mipaka yake, huku wakihimiza amani endelevu, usalama na maendeleo katika taifa hilo.
Kwa kutambua mchango wa wanajeshi wa SAMIDRC, DRC ilitoa shukrani kwa wanaume na wanawake waliotumwa kulinda amani, ikiwapongeza kwa ujasiri na kujitolea kwao katika kuimarisha usalama wa taifa hilo.
Katika hatua nyingine, mkutano huo uliipongeza Jamhuri ya Madagascar kwa kuahidi kutoa msaada wa matibabu kwa waathirika wa mashambulizi na wakimbizi wa ndani waliokimbia makazi yao kutokana na mapigano.
Ponyezo kwa Viongozi wa SADC
Viongozi wa SADC walimpongeza Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake madhubuti na mchango wake katika masuala ya amani na usalama ndani ya jumuiya hiyo.
Aidha, wajumbe wa mkutano huo walipitisha azimio la kumshukuru Mwenyekiti wa SADC, Dk. Emmerson Mnangagwa, kwa kuitisha mkutano huo wa dharura na kwa juhudi zake katika kukuza ushirikiano wa kikanda kwa ajili ya amani na utulivu wa ukanda wa SADC.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED