WAKAZI watatu wa kijiji cha Bashnet, Babati mkoani Manyara, wamefariki dunia kwa madai ya kunywa pombe kali ambazo bado hazijulikani zinakozalishwa huku Jeshi la Polisi likizuia kuzikwa kwa watu hao mpaka uchunguzi ukamilike.
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara Ahmed Makarani, jana alikiri kutokea vifo vya watu hao.
"Tunayo hiyo taarifa tunaendelea na upelelezi hatua za msingi tumeshazifanya sisi hatutazami wapi zinazalishwa bali tunatazama chanzo cha kifo ndiyo tunatafuta chanzo," alisema Makarani.
Aidha, alisema wanasubiri taarifa ya uchunguzi wa daktari kama ni sumu au alikunywa bila kula.
"Ndiyo maana tunafanya uchunguzi wa kina ambapo atafanya daktari na mkemia mkuu wa serikali na wanaweza kutoa mapafu ili wajiridhishe kama ni pombe au sumu," alisema.
Makarani alisema hawawezi kuruhusu kufanyika maziko mpaka wafanye uchunguzi wa kina.
Alisema miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Babati kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Bashnet, Martin Akonay, akizungumzia suala hilo alikiri kutokea kwa vifo vya watu hao. Alisema wote watatu vifo vimefanana.
Akonay alisema historia ya marehemu hao ni wanywaji sana wa pombe huku akidai mmoja alikufa saa 10:00 Alfajili, wa pili saa 3:00 asubuhi na wa tatu saa 9:00 alasiri.
Mwenyekiti huyo alisema wanasubiri matokeo ya uchunguzi utakaofanywa na daktari na mkemia mkuu ili taratibu za mazishi ndio ziweze kuendelea.
Mmoja wa ndugu wa marehemu ambaye hakuwa tayari kuandikwa majina yake aliiambia Nipashe kuwa walikuwa watano hivyo walikimbizwa hospitali na wawili waliokolewa kwa kutolewa sumu mwilini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED