SERIKALI imesema kwa mwaka 2024 iliwapokea na kuwapa huduma jumla ya wanawake na wasichana 213, 675 waliopata changamoto ya kuharibika kwa ujauzito nchini.
Vilevile, serikali imeliarifu Bunge kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2022 hadi 2024, wanawake 92 walipoteza maisha kutokana na changamoto mbalimbali zilizosababishwa na kuharibika kwa ujauzito.
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, alisema hayo jana bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Fatuma Toufiq, aliyetaka kujua idadi ya wasichana na wanawake walioathirika na utoaji mimba usio salama nchini.
Akijibu swali la mbunge huyo, Dk. Mollel alibainisha kuwa kati ya wagonjwa 213,675 waliopatiwa matibabu baada ya ujauzito kuharibika mwaka 2024, wasichana 181, 071 walipatiwa huduma na kuruhusiwa kama wagonjwa wa nje na 32,512 walipatiwa huduma wakiwa wamelazwa.
Takwimu rasmi za Wizara ya Afya zinaonesha kuwapo wastani wa wanawake milioni mbili wanaoshika ujauzito kila mwaka, wakijifungua watoto milioni 2.4 (baadhi yao hujifungua watoto pacha).
MIMBA ZA KUBAKWA
Mbunge Fatuma pia alitaka kauli ya serikali kuhusu wanawake wanaobakwa na kupata mimba zisizotarajiwa.
Akijibu swali hilo, Dk. Mollel alisema kuna haja kutoa elimu ya saikolojia kwa wasichana na wanawake wanaopitia kadhia hiyo na kuhakikisha jamii inapewa elimu vya kutosha ili kuepuka tabia hizo kujitokeza.
“Sisi tuwe mabalozi kwenye jamii kuhakikisha eneo hili la wanawake kunyanyaswa na kubakwa hayatokei kwenye jamii yetu," alisema Dk. Mollel pasi na kutaja idadi ya wanaokumbwa na ukatili huo nchi, kama ilivyohojiwa na mbunge.
Alisema serikali imekuwa na mkakati endelevu wa kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa jamii na kusogeza huduma karibu na wananchi. Mpaka sasa imeshajenga zaidi ya vituo 480 ili kurahisisha upatikanaji huduma hiyo.
Mbunge wa Viti Maalum, Dk. Tea Ntala, alihoji mkakati wa serikali kuhakikisha kuwa matumizi ya dawa za kuzuia kupata ujauzito, maarufu P2, yanaelezwa vizuri ili wasichana wasiathirike ikiwamo kukosa watoto.
Akijibu swali hilo, Dk. Mollel alisema serikali imeshaanzisha kampeni maalum iliyopewa jina la ‘Holela Holela Itakukost’ iliyolenga kutoa elimu kuhusu matumizi mabaya ya dawa, zikiwamo P2.
Aliwaomba wabunge kuendelea kuhimiza kuhusu matumizi mabaya ya dawa, zikiwamo P2, ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CHADEMA), Aida Kenan, alihoji kama serikali imefanya tathmini ya kugundua kiini cha utoaji mimba usio salama.
Akijibu swali hilo, Dk. Mollel alisema suala hilo linasababishwa na kutokuwa na elimu na linaigharimu serikali kwa sababu wengi wanazitoa, wanafikishwa hospitalini wakiwa na hali mbaya na hawana fedha za matibabu, hivyo wanatibiwa pasipo kulipia.
Alisema kuna haja kutoa elimu kuanzia shule za msingi na kuendelea kuhusu madhara ya utoaji mimba.
Naibu Waziri Mollel alidokeza lingine la ziada kwamba wakati mwingine wanawake walioolewa wamekuwa wanatoa mimba wanapogundua kuwa siyo za waume zao.
“Lakini pia wakati mwingine kinamama inatokea amebeba mimba ambayo anajua siyo ya mume wake na inatokea mambo kama hayo (anaitoa)," alisema.
Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Felister Njau, alihoji lini serikali itakuja na sheria ya kumlinda mwanamke ambaye amepata mimba isiyotariwa kama vile kubakwa na ndugu.
Katika majibu yake kwa swali hilo, Dk. Mollel alisema sheria za kumlinda mwanamke anayepitia kadhia hiyo zipo ila kuna haja ya kuelimisha jamii ili kuongeza uadilifu, utu na upendo. Itasaidia kuepuka "majanga kama hayo".
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED