TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani hapa imebaini kuwapo kwa mianya ya upotevu mkubwa wa mapato wakati wa kutoa huduma katika Stendi Kuu ya Msamvu ya Mabasi yaendayo Mikoani.
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa humo, Christopher Mwakajinga, aliyasema hayo jana wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba, 2024.
Mwakajinga alisema mianya ya upotevu wa mapato iliyobainika ni wakusanyaji mapato kutotoa stakabadhi kwa baadhi ya abiria au kutoa zilizotumika.
“Mianya mingine ni kutotoa stakabadhi kwa madai ya kukosekana kwa chenji, wakusanya ushuru kupewa rola chache za stakabadhi zisizoendana na makisio ya makusanyo kwa siku husika,” alisema.
Mwakajinga alisema baada ya kupata taarifa ya kuwapo kwa miaya hiyo walifanya ufuatiliaji wa ukusanyaji wa mapato katika Stendi ya Msamvu kwa siku tatu mfululizo kilichoanzia Desemba 24, mwaka jana kwa saa 24.
Alisema katika kipindi hicho mapato yaliyokusanywa yalikuwa ni Sh. milioni 18.083, ambapo Desemba 12, mwaka jana zilipatikana Sh. milioni 5.6 siku iliyofuata (Desemba 13), Sh. milioni 6.4 na siku ya mwisho (Desemba 14) kiasi kilichokusanywa kilikuwa ni Sh. milioni 5.9.
“Katika tathmini iliyofanyika kwenye ukusanyaji wa mapato kwa mwezi Desemba, mwaka jana, inaonesha makusanyo yaliyopatikana katika siku hizo tatu ndiyo yalikuwa mapato ya juu zaidi kukusanywa kwa mwezi husika,” alisema Mwakajinga.
Alisema ufuatiliaji huo ulibaini kuwapo kwa mianya ya upotevu wa mapato kwa huduma zinazotolewa katika stendi kuu na kwamba, mianya hiyo isipozibwa mapato yatazidi kupotea kwa kuishia mikononi mwa wajanja wachache.
Alisema TAKUKURU Mkoa imeamua kuwa mchakato wa ufuatiliaji mapato katika vyanzo vyote vya ndani ikiwamo kwenye stendi hiyo kuwa endelevu.
Alisema kwa kushirikiana na Manispaa ya Morogoro inafanyia kazi yale yote yaliyobainika katika mchakato husika ili kuweza kuwabaini wahusika wote waliomo katika mnyororo mzima wa ufujaji wa mapato katika stendi hiyo ili kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Nitoe angalizo kwa halmashauri zote ndani ya Mkoa wa Morogoro kuhakikisha wanasimamia ipasavyo ukusanyaji wa mapato kama inavyopaswa,” alisema Mwakajinga.
Kiongozi huyo aliwakumbusha wananchi wote wanaotumia Stendi ya Msamvu kudai stakabadhi kulingana na huduma wanazopewa.
Mmoja wa wadau wa stendi hiyo ya Msamvu ambaye ni mmiliki wa mabasi yaendayo mikoani, Salum Tembo, alitaka TAKUKURU kuwachukulia hatua kali zikiwamo kuwafikisha kwenye vyombo vya kisheria wahusika wote waliobainika kuwapo kwa upotevu huo wa fedha za serikali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED