Bunge lapitisha azimio kumpongeza Rais Samia Mkutano Nishati Afrika

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 08:30 AM Feb 01 2025
Rais Samia Suluhu Hassan.

BUNGE limempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Nishati Afrika (Mission 300) Mwaka 2025 kwamba, umeiletea sifa ya kipekee Tanzania na kutaja namna Watanzania walivyonufaika.

Akisoma azimio la pongezi hizo bungeni jana, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Asia Halamga, alisema mkutano huo ulikuwa na manufaa makubwa  kwa uchumi wa Tanzania na Bara zima la Afrika.

Alisema wawekezaji katika sekta ya hoteli na malazi, usafiri na usafirishaji, wauzaji wa vyakula na vinywaji, wauzaji wa bidhaa mbalimbali pamoja na sekta ya utalii wamenufaika na Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo.

“Kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano, wafanyabiashara wameweza kutengeneza mtandao katika biashara zao kwa kufanya mazungumzo ya kibiashara, yaani Business to Business na Business to Customer (B2B na B2C) pembezoni mwa mkutano huo na tumeingiza fedha za kigeni, suala ambalo limeleta manufaa makubwa kwa uchumi wa nchi yetu,” alisema.

Alisema mkutano huo umeazimia masuala mbalimbali yakiwamo mataifa mbalimbali yametoa ahadi za mipango ya mageuzi makubwa ya nishati yanayolenga kuimarisha nishati mbadala na jadidifu, kuboreshwa kwa gridi za umeme na kuimarisha upatikanaji wa suluhu ya nishati safi za kupikia.

Pia alisema kuzinduliwa kwa Mipango ya Kitaifa ya Nishati kwa lengo la kuvutia wawekezaji na mageuzi ya sera; kutolewa kwa ahadi za ufadhili kutoka taasisi za kifedha za kimataifa kama vile Benki ya Maendeleo ya Afrika na Benki ya Dunia.

Alisema kuvutia sekta binafsi kuwekeza mitaji katika sekta ya nishati barani Afrika na kufikiwa kwa Azimio la Dar es Salaam, ambalo limelenga kuhakikisha upatikanaji wa umeme kwa watu milioni 300 barani Afrika ifikapo 2030.

 â€śAzimo la Dar es Salaam linamanufaa makubwa kwa Bara la Afrika, kwani kupitia azimio hilo, imekubalika kwamba, upo umuhimu wa kuzingatia usawa wa kijinsia katika kuongeza upatikanaji wa nishati hasa kwa wanawake na wafanyakazi, ili kuimarisha muhstakabali endelevu,”alisema.

Vilevile,  azimio hilo linasisitiza umuhimu wa kuunganisha nishati kati ya nchi za Afrika, kutumia vyanzo vya nishati jadidifu kama jua, upepo, umeme wa maji, nishati za joto ardhi, ili kuwa na mifumo imara ya nishati.

Alisema wanampongeza Rais Samia kwa mafanikio hayo na kuhudhuriwa na wageni takribani 2,600 wakiwamo wakuu wa serikali na nchi takribani 21 kutoka barani Afrika, mawaziri na viongozi mbalimbali wa taasisi za kimataifa za fedha na nishati na wadau wengine.

Mbunge huyo alisema mkutano ulikuwa wa weledi na viwango vya hali ya juu kimataifa kutokana na uratibu mzuri uliofanywa na serikali anayoiongoza.

“Rais Samia ameonesha nia ya dhati kuhakikisha kuwa ifikapo 2030, asilimia 75 ya Watanzania watakuwa wamepata nishati safi ya kupikia na hatimaye kufikia 2034, Watanzania wote wawe wamepata nishati safi ya kupikia,” alisema.

KISHOA AGUSWA

Akichangia azimio hilo, Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Jesca Kishoa, alisema anaungana na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa uamuzi wa kumpitisha Samia kuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba,  mwaka huu, kwa maono aliyo nayo kwenye nishati, uchumi na diplomasia.

Alisema Rais Samia amefanya kazi ya kuimarisha diplomasia, uchumi na kuwa kinara wa matumizi ya nishati safi.

“Kwa haya yaliyofanyika mkutano mkuu na mengine haya mambo yamehalalisha uamuzi wa mkutano mkuu wa CCM yaliyofanyika mwaka huu na mimi ninaungana kwa asilimia 100 kwa uamuzi wa wajumbe wa CCM walioufanya,” alisema.