Baada ya Nipashe kutoa ripoti ya uchunguzi iliyoonesha ni kwa namna gani hali ya rushwa kwa askari wa usalama barabarani ilivyokithiri mkoani Kigoma. Jeshi la polisi mkoani humo limewashikilia askari wawili wa kikosi cha usalama barabarani walioonekana katika picha mnato na jongefu wakipokea rushwa katika kituo cha ukaguzi wa magari Kazegunga.
Katika sehemu hii, ripoti inaweka wazi kilichonyuma kukithiri kwa vitendo vya rushwa kwa askari wa usalama barabarari na si tu mkoani Kigoma bali maeneo yote nchini.
ASKARI WALIVYONASWA
Taarifa iliyotolewa Januari 27, mwaka huu, na msemaji wa Jeshi la Polisi mkoani Kigoma, Philemon Makungu, ilieleza kuwashikilia askari wawili wa kikosi cha usalama barabarani walioonekana kushiriki vitendo visivyo na maadili, kinyume cha Sheria ya Usalama Barabarani kupitia video iliyorushwa katika mtandao wa kijamii wa gazeti hili.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa watuhumiwa waliokamatwa wako mahabusu na hatua za kinidhamu zinaendelea dhidi yao kabla ya hatua zingine za kisheria kuchukuliwa.
Vilevile, taarifa hiyo inaeleza namna ambavyo askari hao wamechafua taswira ya Jeshi la Polisi na kwamba jeshi hilo halitavumilia ukiukwaji wa maadili na sheria, hivyo litaendelea kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria dhidi ya askari wanaokiuka maadili ya utendaji kazi.
MAONI YA WADAU
Wadau wa masuala ya usalama barabarani wanasema Jeshi la Polisi halichafuliwi taswira na askari hao bali ni mfumo walioukuta na kuuendeleza kutokana na mifumo mibovu ya sheria pamoja na usimamizi mbovu wa sheria zilizopo.
Aidha wanasema mifumo mibovu ya sheria ndicho chanzo cha kutozingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, hivyo kusababisha kukithiri kwa rushwa kati ya matrafiki na madereva wa mabasi, yakiwamo ya daladala wanaotoa huduma za usafiri mkoani Kigoma na maeneo mengine nchini.
Wanasema sheria zimenyimwa meno na mamlaka zinazoshughulikia masuala ya rushwa barabarani zimeshindwa kuwashughulikia watuhumiwa kama wanavyoshughulikia makosa mengine ya jinai.
Ibrahim Sadick, Mkuu wa Kitengo cha Elimu kwa Umma kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kigoma, anasema taasisi hiyo haina mamlaka kamili ya kukamata kwa mujibu wa sheria.
Anasema hawana mamlaka ya kutuhumu, kukamata, kuchunguza na kupeleka watu mahakamani, kwa kuwa utaratibu huo unakiuka mnyororo wa haki jinai na kwamba ili kufanikisha hilo lazima awapo mtu anayeshtaki ili kuepuka uonevu.
Pia anasema hakuna mtu aliyewahi kushtakiwa kwa kosa la kutoa au kupokea rushwa barabarani kwa madai kuwa chanzo ni kukosekana kwa ushahidi.
“Hatujapokea kesi ya mtu aliyefungua madai juu ya rushwa barabarani. Malalamiko yanakuja lakini hayafunguliwi kama kesi rasmi. Tunahitaji ushirikiano wa wananchi kwa kufungua madai. Hatuwezi kuchukua hatua bila ushahidi,” anasema Sadick.
Wakili Thomas Masasa kutoka Msasa Law Chamber anaangalia tatizo la mfumo kwa namna ambavyo TAKUKURU na Jeshi la Polisi wanavyopaswa kushirikiana ili kuondoa tatizo hilo.
Anasema marekebisho ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Oktoba 2024, yanawapa mamlaka ya kushtaki baadhi ya makosa yanayohusiana na rushwa bila kupata kibali kutoka kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali.
Anasema kuna changamoto ya vitendea kazi na idadi ya maofisa uchunguzi wa TAKUKURU kulinganisha na ile ya askari wa usalama barabarani, hivyo inakuwa ngumu kwa maofisa hao kupambana na vitendo vya rushwa barabarani.
“Ofisi nyingi za TAKUKURU zina wafanyakazi wachache. Unaweza kukuta maofisa watatu katika wilaya nzima wakati polisi wapo mara tatu yao. Watawezaje kuwakabili?” anahoji.
Anasema maofisa haohao ndio wanatakiwa wapambane na rushwa za halmashauri na taasisi zingine, hivyo inawawia vigumu kuwapo kila eneo kuzuia rushwa. Kwa mantiki hiyo, anasema wanahitaji wananchi kutoa ushirikiano dhidi ya vitendo vya rushwa barabarani.
Ripoti ya Uchambuzi wa Mfumo wa Utendaji Kazi wa Askari wa Usalama Barabarani ya Machi 2023 iliyofanywa na TAKUKURU mkoani Kigoma inabainisha kuwa baadhi ya madereva wa viongozi hukwepa sheria kwa kisingizio cha “simu moja tu.”
Katika uchambuzi huo, ilionekana kuwa wanaoonewa na kuguswa na fedha ya rushwa ni wale wasioendesha magari ya wanaodaiwa kuwa viongozi wenye nyadhifa serikalini. Endapo dereva wa aina hiyo atakamatwa na kosa la usalama barabarani, akipiga simu kwa mwajiri wake mara nyingi askari aliyemkamata hupewa maelekezo ya kumwachia dereva.
Vilevile, ripoti hiyo inaonesha kuwa madereva wanaofanya kazi kwa mazoea, huamini kuwa ‘pesa ya ushirikiano’ inaweza kumaliza kila tatizo, hali ambayo inawakatisha tamaa askari waadilifu.
Wakili Msasa anasema madereva wamekuwa wakiwashawishi matrafiki kupokea ‘pesa ya ushirikiano’ kwa kuwa wengi magari yao hayajakamilika, hivyo kuliko kutoa faini ya Sh. 30,000 wanaona ni bora kutoa Sh. 2,000 kinyume cha sheria.
SABABU KUKITHIRI
Ripoti ya Utafiti wa Rushwa (2020) inaonesha kuwa madereva wa daladala mara nyingi hutumia rushwa kuepuka adhabu.
Dereva wa daladala za Simbo ambaye hakutaka jina lake kutajwa anasema madereva wengi hawana uelewa wa kanuni za usalama barabarani, huku wakitegemea mfumo uliopo ambao huruhusu ‘ushirikiano’ ili waendelee kufanya biashara.
“Tunaumizwa kwa kuwa hatujui sheria za usalama barabarani kwa hiyo mkoa umeamua kutumia huo udhaifu ili kupata pesa za ziada wakijua hakuna wa kuwashtaki,” anasema dereva huyo.
Dereva Juma Juma anasema shida ya kuendelea kwa rushwa kati ya madereva wa daladala na askari wa usalama barabarani ni woga wa madereva kwa kuwa kuna kipindi wanakuwa na magari mabovu, hivyo kuwapasa kutoa ‘ushirikiano’ ili wasikamatwe na waendelee kufanya kazi.
“Wakati mwingine tunaogopa kwa sababu hii pesa inayotolewa haitolewi kwa siri tena na mnaweza kugombana na askari mbele ya abiria ikiwa dereva atagoma kutoa hiyo pesa, unafikiri wanajiamini na nini? Maana ndani ya gari kuna watu wengi na wao hawajali hii hali ina kitu kinachowafanya kuwa majeuri na kuhisi pesa hiyo ni haki yao” anasema Juma.
Dereva mwingine, Liberatus Dotto, anasema wanatoa rushwa kwa sababu vizuizi vimewekwa kimkakati na kufanya hivyo ni nafuu zaidi kuliko kulipa faini ya Sh. 30,000 kwa kila kosa.
Katibu wa Jumuiya ya Maridhiano Mkoa, Shukuru Kondo, anasema madereva mara nyingi hukwepa uwajibikaji kwa kujaza abiria kupita kiasi au kutumia magari mabovu, hali inayowafanya kutoa rushwa.
Anasema aliwahi kuwahoji madereva kwa nini wanatoa rushwa na kusababisha makosa ya usalama barabarani kwa makusudi na walimjibu kuwa rushwa haiepukiki kwa kuwa wanatafutiwa makosa na kwamba hata kama gari limekamilika kwa asilimia 100 askari watatafuta kosa lolote ili mradi tu madereva wakutwe na hatia.
Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Mkoa wa Kigoma, Frank Makua, anapendekeza sheria iweke wazi juu ya uwapo kwa jengo la pamoja kwa ajili ya polisi, Wakala wa Misitu (TFS) na Halmashauri ili kupunguza vizuizi na urasimu vinavyochangia rushwa kwa sababu anaamini vizuizi vyote vinafanya kazi moja.
Naye mwananchi, Peter Bwenga anasema anachokiona ni maelekezo kutoka mamlaka za juu kwa kuwa jambo hili liko wazi na viongozi wa mkoa wanaona yanayotendeka barabarani na anaamini kwamba wangeamua kufanya jambo kutokomeza ‘ushirikiano’ wangeweza kwa kuwa serikali haijawahi kushindwa kitu.
Kiongozi wa KIBOTA, jina tunalo, anasema tatizo la rushwa barabarani linasababishwa na usimamizi mbovu wa sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa akitaja namna ambavyo taasisi moja ya haki za binadamu ilivyoanza kuingia barabarani kutafuta haki za binadamu na kisha kuomba pesa kutoka kwa madereva.
“Barabarani hatuongozwi na sheria. Sheria inakuja tu pale dereva anapokosea, hivyo tunaongozwa na hisia za watu. Kuna siku nimeona watu waliojitamblisha kuwa wa haki za binadamu wakidai abiria amenyimwa haki yake kwa kupakata mzigo wake mdogo akiwa ndani ya gari baada ya hapo wakataka tuwape fedha. Yaani kila mtu ameona barabarani ndiyo sehemu ya kuchuma pesa” anasema.
Mfanyabiashara Mwasiti Ramdhani anasema chanzo cha ukiukwaji wa sheria ya usalama barabarani ni njaa kwa matrafiki, akianisha kuwa kuna kipindi wanawaomba madereva wawapitishie maji au chakula na kwamba kuna kipindi wanaomba hata kupewa Sh. 1,000 ilimradi tu wapate pesa ya kukidhi mahitaji yao.
NANI AWAJIBIKE?
Wakitoa maoni ya nani awajibike juu ya utekelezaji mbovu wa sheria hizo, Kemon Obedy anasema serikali inapaswa kuwajibika kwakuwa wanaoumia ni wananchi ambao ni walipa kodi wake, hivyo inapaswa kuingilia kati kukomesha suala hilo.
Hamis Shomari anasema mamlaka zote zinazotekeleza masuala ya usalama barabarani zinapaswa kuwajibika kwa kuwa kinachoendelea kwa namna moja au nyingine wao ndio wasababishi wakuu.
Sheila Shaban anasema wananchi wawajibishwe kwa kushindwa kutoa taarifa za rushwa barabarani kwa mamlaka husika na kwamba wananchi ndio wanaolea ugonjwa huo mbaya.
Itaendelea…..
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED