WATAALAM wa afya wamebainisha kwamba ugonjwa wa chuki hasi ni moja ya ugonjwa hatari wa kuambukiza na unaoleta madhara na kuuwa kwa kasi katika jamii.
Mtaalamu wa Maendeleo ya Binadamu na Mbobevu wa Afya Bora ya Akili, Dk. Mayrose Majinge, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Siku ya Tuzo za Kizalendo.
Dk. Majinge alisema ugonjwa huo unamaliza na kuua kwa kasi ya juu bila kujua na wengi wao hawatambui kama wanasumbuliwa nao, hali inayofanya kushindwa kujitibia na kupata suluhu ya matibabu na kupona.
Alisema ugonjwa huo unaua kwa kasi kubwa kuliko magonjwa hatari duniani na kupunguza kinga ya mwanadamu kwa haraka.
Mtaalamu huyo alifafanua chuki yaweza kuwa hasi au chanya kulingana na namna inavyotumika na kuchukuliwa, huku akitolea mfano wa mtu anapata maambukizi kupitia rushwa, vurugu, ubaguzi wa rangi, kutovumilia mambo au matukio ya unyanyasaji wa kijinsia.
Alisema jopo la wataalamu waliofanya utafiti walibaini wengi wanakumbwa na ugonjwa huo kutokana na ukosefu wa upendo miongoni mwa mtu na mtu katika jamii iliyowazunguka ikiwamo kuchukiana au kutokupendana.
Alisema kutokana na hali hiyo huku Watanzania wengi wakionekana kuwa ni waathirika wameamua kuja na tuzo uzalendo zitakazoweza kusaidia watu kupendana ili kuondoa chuki baina ya mtu na mtu pasipo sababu.
“Unakuta mtu anamchukia mwenzie bila sababu za msingi, mwingine anajikuta anatamka kabisa fulani simpendi. Huyu ana viashiria vyote kuwa ni mgonjwa wa chuki, asipojitibia kwa wakati anajikuta ugonjwa huo unammaliza pasipo kujua,” alisema.
“Februari 13, mwaka huu, viongozi mbalimbali wa kitaifa, watu mashuhuri watakutana ili kutoa elimu ya kujitibia na kukabiliana na mmomonyoko wa maadili na kuepukana na chuki hasi.
Baada ya taarifa hiyo, Nipashe ilipozungumza na baadhi ya wananchi mtaani wakiwamo Joyce Peter na Peter Mathias, wote wakazi wa Kinondoni, Dar es Salaam, walisema hawatambui kama kuna ugonjwa wa namna hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED