MABINGWA watetezi, Yanga wamekaa kileleni baada ya kuwaangamiza Kagera Sugar mabao 4-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam jana.
Ulikuwa ni ushindi wa sita mfululizo kwa Yanga tangu ilipopoteza kwa kufungwa mabao 3-1 dhidi ya Tabora United, Novemba 7, mwaka jana, pia ikiwa chini ya Kocha Mkuu, Mjerumani, Sead Ramovic.
Ushindi huo unaifanya Yanga kufikia pointi 42 baada ya kucheza michezo 16, ikishinda mechi 14, ikipoteza miwili, huku ikiendelea kuwa timu pekee ambayo haijapata sare yoyote mpaka sasa msimu huu.
Hata hivyo, kuendelea kujidai kileleni kwa Yanga kutatokana na matokeo ya mchezo wa leo, kati ya Simba itakayoshuka ugenini kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora kuvaana na wenyeji, Tabora United.
Iwapo Simba itashinda, Yanga itashuka tena kwenye nafasi yake ya pili, lakini itaendelea kutamba kileleni kama Wekundu wa Msimbazi, wenye pointi 40, watapoteza au kutoka sare.
Katika mchezo huo, shambulizi la kwanza lilianza dakika ya pili ya mchezo, Yanga ikiingia ndani ya eneo la wapinzani wao kwa mpira uliporwa na Mudathir Yahaya kutoka kwa mabeki wa Kagera Sugar, akaupeleka kwa Stephane Aziz Ki, ambaye shuti lake lilionekana linajaa ndani ya nyavu na mashabiki kunyanyuka, lakini lilitoka juu kidogo ya lango.
Shambulizi lingine la hatari lilifanywa na Yanga dakika ya 15, wakati Aziz Ki, alipowatoka mabeki wa Kagera Sugar, akammegea, Clement Mzize ambaye shuti lake lilitoka pembeni kidogo ya lango.
Mabeki wa Kagera Sugar wakijitahidi sana kuzima mashambulizi ya Yanga upande wa kushoto kutoka kwa Shadrack Boka.
Akishirikiana na beki wake wa kati, Abdallah Mfuko, walifanya kazi ya ziada na kama si uzembe wa baadhi ya wenzao, mechi hiyo ingeenda suluhu mapumziko. Hata hivyo kazi hiyo ilifanikiwa kipindi cha kwanza tu.
Mzize aliwanyanyua mashabiki wa Yanga dakika ya 31, waliokuwa wamekaa muda wote wakiwa hawaelewi, alipopachika bao la kwanza lililotokana na makosa ya mabeki wa Kagera Sugar ambao walianza mpira kizembe ambao ulinaswa, ukapelekwa kwa Aziz Ki, ambaye hakuwa mchoyo, anamwekea mfungaji huyo aliyekuwa katika nafasi nzuri ya kupachika bao.
Lilikuwa ni bao la saba kwa Mzize msimu huu, lakini wakishuhudia Aziz Ki, akikosa penalti dakika ya 35, kufuatia kipa wa Kagera Sugar, Ramadhani Chalamanda, kuipangua na ulipotua katika mguu wa kulia wa Israel Mwenda, alipiga nje.
Penalti hiyo ilitolewa na mwamuzi, Nassor Mwinchui, baada ya Hijja Shamte, kumwangusha Mudathir Yahya, ndani ya eneo la hatari.
Kipindi cha pili ndipo dhahama ilipowaangukia Kagera Sugar, Mudathir alipachika mpira wavuni dakika ya 59, kufuatia kuunganisha vyema krosi ya Prince Dube huku Pacome akifunga bao la tatu dakika ya 77, baada ya mwamuzi, Nassor Mwinchui, kutoa penalti nyingine, pale, Maxi Nzengeli alipoangushwa ndani ya eneo la hatari.
Kennedy Musonda alifunga bao la nne dakika tano kabla ya mchezo kumalizika akiunganisha krosi kutoka wingi ya kulia, iliyotokana na kona fupi ambayo iligongwa na wachezaji kadhaa kabla ya kumiminwa langoni, mfungaji akitumia tena makosa ya walinzi wa Kagera Sugar na Chalamanda kutegeana kuondoa hatari hiyo.
Kagera Sugar yenye pointi 11 inaendelea kubakia nafasi ya 15 ya msimamo wa Ligi Kuu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED