WASANII wanaoshiriki kampeni ya kutoa elimu ya fedha kwa wananchi kutoka Shirika la Kijamii linalojishughulisha na utoaji wa Elimu ya Uraia (TACCI), lililopata semina ya elimu hiyo, wametakiwa kuwa mfano kwa jamii kwa kuzingatia sheria na kanuni za uendeshaji wa shughuli hizo.
Hayo yameelezwa mkoani Morogoro na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Janeth Hiza, wakati akifunga Mafunzo ya Elimu ya Fedha kwa Wasanii, yaliolenga kutoa elimu hiyo kwa njia bunifu ya sanaa.
“Wizara ya Fedha tunajipanga kwenda vijijini kutoa elimu ya fedha, kwa kuwatumia wasanii wa ngoma, nyimbo na maigizo na tunatamani kuona wananchi wengi zaidi wanafikiwa kwa njia rahisi lakini yenye ufanisi’’ alisema.
Amewataka wasanii kuendelea kubuni sanaa zinazoelimisha jamii kwa kuwa kazi za sanaa zinamvuto na hazichoshi kuzisikiliza na kuzitazama, hivyo zikitumiwa kwa malengo chanya zitatoa mchango mkubwa katika kusukuma gurudumu la maendeleo nchini.
Akizungumza kwa niaba ya wasanii wa Shirika la Kijamii linalojishughulisha na utoaji wa Elimu ya Uraia (TACCI), Mtaalam wa Sanaa za Jukwaani, Harrison Kisaka, alisema kuwa elimu waliyoipata mwanzo ilikuwa na lengo la kuisaidia jamii hasa vijijini, lakini imekuwa msaada mkubwa kwa wajumbe wote wa mafunzo hayo, hivyo akaahidi kuwa watakuwa chachu ya uelewa wa elimu hiyo kwa jamii inayowazunguka.
Alisema kuwa pamoja na mambo mengine watatumia muda mrefu kuigiza, kuimba na kubuni sanaa ya ngoma zitakazojikita kwenye elimu ya fedha ili na wao waweze kutoa mchango wao kwa taifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED